WATU WANANE WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA KUTUPA VIUNGO VYA BINADAMU HUKO BUNJU.

Na Rose Masaka-MAELEZO_DAR ESALAAM
 
JESHI la Polisi Kanda ya Dar es Salaam linawashikilia  na kuwahoji watu wanane kwa kutupa  viungo vya binadamu katika bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju wilayani Kinondoni .
 
Kamishna wa Polisi  Kanda Maalum ya Dar es Salaan  Suleiman Kova amesema hayo leo Ofisi kwake wakati wa mkutano na waandishi wa habari .
 
Amesema kuwa watu hao wakimemo madaktari wa International Medical and Technological University (IMTU) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukiri kuhusika na tukio la utupaji wa  viungo  vya binadamu katika eneo hilo.
 
Kamishna Kova amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwahoji na kufanya uchunguzi kuona kama wahusika wamefanya kosa  linalohitaji kuchukuliwa hatua za kisheria au hawana kosa.
 
Ameongeza kuwa kufuatia tukio hilo tayari Jeshi la Polisi Kanda Maalum limeshafungua jarada la uchunguzi kubaini ikiwa wahusika wametenda kosa linalohitaji kufikishwa kwenye vyombo vya sharia kwa hatua zaidi.
 
Kamishna huyo amesema kuwa katika kutekeleza jambo hilo tayari jopo la wachunguzi likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam  Jaffar Mohamed linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha watu hao kutupa viungo hivyo katika eneo hilo na idadi ya watu kulingana na viungo vilivyotupwa
.
Aidha Kamishna Kova amewasihi wananchi wasiwe na wasiwasi kwani viungo vilivyookotwa  havina uhusiano na mauaji ya watu wengi na wala havihusiki na masuala ya ushirikina.
 
Amewaahidi wananchi kutoa taarifa kamili mara tu upepelezi utakapokamilika.
Viungo vya binadamu vikiwemo mikono, miguu, vichwa , mapafu na mioyo viligundulika jana (21.7.2014) jioni vikiwa vimehifadhiwa katika mifuko ya plastiki 85 na kutupa katika bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju wilayani Kinondoni.
 
Mara baada ya kugunduliwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni walivichukua na kuvipeleka katika Hospitali ya Taifa kwa uchunguzi zaidi.

Post a Comment

Previous Post Next Post