Zaidi ya watu elfu moja waliuawa wakipinga kuondolewa kwa Morsi.
Serikali ya Misri imewanyima vibali vya kuingia nchini humo maafisa wawili wa kupigania haki za kibinadamu ikihofia usalama wao.
Mkurugenzi mkuu Kenneth Roth na bi Sarah Leah Whitson walikuwa mjini Cairo kuzindua ripoti maalum kuhusiana na mauaji yaliyotokea wakati wa maandamano yaliyopelekea kupinduliwa kwa serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Mohammed Morsi.
Mamia ya watu waliripotiwa kufariki mnamo tarehe 14 Agost1 2013 baada ya maafisa wa Usalama kutibua maandamano ya kupinga kung'olewa madarakani kwa Morsi.
Rais Abdul Fattah al-Sisi, alikuwa mkuu wa majeshi wakati huo yalipotokea mauaji hayo.
Shirika hilo la Human Rights Watch (HRW) lilikuwa mstari wa mbele kushtumu mauaji ya wapinzani wa serikali kufuatia kung'olewa madarakani kwa Morsi mwezi Julai mwaka uliopita.
Mkurugenzi mkuu wa HRW Kenneth Roth na bi Sarah Leah Whitson waliondolewa Misri.
''Kwa sababu ya hofu ya Usalama wao Maafisa hao wawili walikamatwa kwa takriban saa 12 kabla ya kurejeshwa makwao '' afisa mmoja wa usalama ambaye hakutaka kutajwa jina lake aliiambia BBC.
Bi Whitson,ambaye ni afisa mkuu wa HRW katika eneo la Mashariki ya Kati alisema kuwa walielezwa kuwa walikuwa wakifurushwa nje ya Misri kwa sababu za kiusalama.
Kulingana na HRW hii ndiyo iliyokuwa mara ya kwanza kwa maafisa wao kunyimwa ruhusa ya kuingia ndani ya Misri hata wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak.
Katika ripoti hiyo itakayozinduliwa hapo kesho tarehe 12.o8.2014 " maafisa wa polisi na jeshi la Misri walifyatulia waandamanaji risasi " haswa baada ya kung'olewa madarakani kwa aliyekuwa rais Morsi.
Zaidi ya watu 1,150 waliuawa katika maandamano 6 kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka uliyopita.
Maafa zaidi yaliripotiwa katika medani ya Nahda na karibu na Msikiti wa Rabaa al-Adawiya ulioko Cairo.
.Shirika la Human Rights Watch linakusudia kutoa ripoti ya ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini Misri.
Bwana Roth aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa Tweeter kuwa ''mauaji yaliyofanyika katika msikiti na medani ya Rabaa ni sawa tu na yale yaliyotokea huko Tiananmen na Andijan" lakini serikali ya Misri imeninyima ruhusu ya kuzindua ripoti itakayosimulia yaliyojiri huko.
Roth alisema kuwa Human Rights Watch ilikuwa imekwisha iarifu utawala wa Misri kuhusu ripoti hiyo na ilikuwa inatarajia kujadiliana na serikali ya rais Sisi.
Serikali haijapinga wala kukubali madai hayo.
Post a Comment