Kutoka kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa UN Women
nchini Tanzania, Anna Collins, Meneja wa Haki za Watoto kutoka Graca Michel
Trust, Bernard Orimbo na mwakilishi wa asasi za Mkoa wa Mara.
SERIKALI kupitia Wizara ya
Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na mashirika na asasi
anuai zinazotetea haki za watoto na jamii kwa ujumla imezinduwa kampeni maalumu
za kitaifa za kupinga ndoa za utotoni (National Ending Child Marriage Campaign)
ambazo zimekuwa zikikwamisha haki ya elimu kwa mtoto wa kike.
Uzinduzi huo umefanyika leo
jijini Dar es Salaan kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi
ya Watu (UNFPA), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Shirika lisilo la
Kiserikali la Children’s Dignity Forum (CDF), Graca Machel Trust (GMT), asasi
za mkoani Mara na uongozi wa mkoa huo.
Akizungumza katika uzinduzi
huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna Maembe
alisema Serikali ipo kwenye mchakato wa kupitia sheria zake ikiwemo Sheria ya
Ndoa ya Mwaka 1971 ambayo imekuwa na utata juu ya umri wa kuolewa kwa mtoto wa
kike.
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, pamoja na mambo mengine inaruhusu mtoto wa
kike miaka 14 au 15, kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au mahakama jambo ambalo
linatajwa na wanaharakati kuwa kikwazo cha elimu kwa mtoto huyo.
Akifafanua zaidi Katibu Mkuu
aliwahakikishia washiriki wa mkutano huo kuwa sheria hiyo itabadilika hasa
baada ya mchakato wa katiba kukamilika hivyo kuwataka wananchi kwa kushirikiana
na asasi anuai kuunga mkono juhudi za kupinga ndoa za utotoni zinazoendekezwa
kwa baadhi ya maeneo nchini Tanzania.
Alisema uwepo wa udhaifu wa
sheria isiwe kisingizio cha kuendeleza vitendo hivyo viovu kwenye jamii kwani
Serikali wakati wote kupitia watendaji wake ipo tayari kupambana na watu
wanaoendeleza vitendo hivyo pale inapofikishiwa taarifa.
“…Jamii lazima ikubali
kubadilika na kuacha vitendo hivi vya kuwaozesha watoto, hivi kati yetu hapa
nani anakubali mtoto wake akatishwe masomo na kuozeshwa? Tukiwa tayari kupiga
vita kuanzia kwenye familia zetu makazi yetu suala hili litakoma…Ni kweli
Serikali ipo kwenye utaratibu wa kuipitia sheria na nawahakikishia itafanyiwa
mabadiliko lakini kama jamii nasi tunatakiwa kubadilika na kuacha vitendo hivi,”
alisema Bi. Maembe.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa TAMWA, Valerie Nsoka alisema shughuli za kampeni hizo maalumu za
kupinga ndoa za utotoni zinatarajiwa kufanyika Mkoani Mara na zitaambatana na
utoaji elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, watendaji wa
vyombo vinavyosimamia sheria,
viongozi wa jamii na jamii kwa ujumla juu ya
mapambano ya kampeni hizo. Alisema kampeni hizo baadaye
zitaendelea katika maeneo mengine ya Tanzania lakini kwa sasa Mkoa wa Mara
ndipo zitakapoanzia na limechukuliwa kama eneo la mfano kwa kuanzia.
“Tunaamini tunaweza kushirikiana na jamii kwa kuwalinda watoto wetu ambao
wamekuwa wakinyimwa haki ya msingi ya kupata elimu na baadhi ya watu,” alisema
Bi. Nsoka.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Children’s Dignity Forum (CDF),
Koshuma Mtengeti akizungumza katika hafla hiyo alisema takwimu zinaonesha
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo inaidadi kubwa ya ndoa za utotoni.
Aliongeza kuwa takwimu zinaonesha kati ya wasichana 5 wanaoolewa Tanzania
wawili kati yao huolewa wakiwa chini ya miaka 18 ilhali sheria ikiendelea kuwa
na utata.
Aidha Meneja wa Haki za Watoto
kutoka Graca Michel Trust, Bernard Orimbo juhudi za makusudi zikifanywa kwa
makundi yote kampeni hizo zinaweza kufanikiwa kwani taasisi hiyo kwa
kushirikiana na Serikali ya Zambia ilipata mafanikio makubwa dhidi ya kampeni
kama hizo zilizoanza kufanyika mwaka 2013.
Imeandaliwa na
www.thehabari.com
Post a Comment