Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Halmashauri ya Geita itaanza kupata wastani wa Dola za Marekani milioni 1.8 kwa mwaka kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) baada ya kusainiwa rasmi kwa marekebisho ya mkataba baina ya kampuni hiyo na Serikali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kabla ya kutiliana saini marekebisho ya mkataba huo ambao uliosainiwa awali mwaka 1999. Awali, Halmashauri hiyo ilikuwa ikipata ushuru wa huduma wa Dola za Marekani 200,000 kila mwaka badala ya kulipwa asilimia 0.3 ya mapato ghafi ya kila mwaka kama sheria ya fedha ya serikali za mitaa ya mwaka 1982 inavyotaka.
Kwa kuzingatia kiwango cha mapato ghafi ya mgodi wa Geita kwa mwaka yanayopatikana hivi sasa, Halmashauri ya Geita itakuwa na uhakika wa kupata kiasi kisichopungua Dola za Marekani milioni 1.8 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na wamiliki wa mgodi huo, malipo hayo yataanza kulipwa rasmi kuanzia tarehe 01 Julai, 2014.
Profesa Muhongo alisema kuwa fedha hizi ni nyingi mno na kuwataka wananchi wa Geita kujiandaa kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu pamoja na huduma za jamii zitakazopelekea uchumi wake kukua kwa kasi.
Profesa Muhongo alisisitiza kuwa ni vyema makabidhiano ya fedha hizo kwa njia ya hundi yakafanyika kwa uwazi mbele ya wananchi ili kupunguza malalamiko, ikiwa ni pamoja na kuongeza imani kati ya wananchi na migodi.
Aidha, aliwataka Viongozi wa Halmashauri hiyo, kusimamia vyema fedha hizo kwa kuhakikisha kuwa zinachangia katika shughuli za maendeleo badala ya kutumika katika matumizi yasiyo ya lazima na tija katika jamii, hususani kulipana posho za vikao na safari.
“ Kwa mazingira ya sasa, mji wa Geita hauna sababu ya kukosa maji, barabara bora, vituo vya afya, ni imani yangu kuwa fedha hizi zitachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Geita iwapo zitasimamiwa ipasavyo,” alisema.
Maeneo mengine yaliyofanyiwa marekebisho kwenye mkataba wa awali uliosainiwa mwaka 1999 ni kupandisha kiwango cha malipo ya mrabaha kutoka asilimia tatu ya mapato baada ya kuondoa gharama za uchakataji madini na kufikia asilimia nne ya mapato ghafi.
Eneo jingine lililofanyiwa marekebisho ni kufuta kipengele kilichokuwa kinatoa nyongeza ya asilimia 15 kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa. Kuendelea kuwepo kwa kipengele hiki kwenye mkataba, kungeipunguzia serikali kodi ya mapato.
Post a Comment