Na Mwandishi wetu
Mbunifu
wa kimataifa wa mavazi kutoka Tanzania, Sheria Ngowi amedhihirisha kuwa
yeye ni nguli katika ubunifu baada ya kufinika katika onyesho la mavazi
la kimataifa lijulikanalo kama Mercedes Benz Fashion Week Africa 2014
lililofanyika juzi Ijumaa mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Ngowi
alionyesha mkusanyiko wa mavazi aliyoyaita ‘PRIDE’ yaani kujivunia,
kama moja ya njia za kumuenzi Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere pamoja
na viongozi mashuhuri waliopigania uhuru Afrika.
Afrika
Kusini ilizizima na kuduwaa kwa muda usiopungua dakika 15 pale ambapo
mavazi mbali mbali yaliyobuniwa na Ngowi yalipokuwa yakioneshwa katika
ukumbi wa Melrose Arch.
Sheria
Ngowi alionyesha mkusanyiko wa mavazi aina ya suti yenye ubunifu na
ueledi wa hali ya juu kwa kutumia vitambaa vya kisasa na kale
vilivyonakshiwa kwa maua na rangi za kuvutia kama nyekundu, zambarau,
machungwa, nyeupe na nyeusi huku mengine yakiwa bila maua lakini
yaliyong’aa kwa kutumia rangi imara kama blu, kahawia na kijivu.
Onyesho
hilo la Mercedes Benz Fashion Week Africa 2014 lilihudhuriwa na watu
mbali mbali wakiwemo viongozi wa umma kutoka Afrika kusini, Balozi wa
Tanzania Afrika Kusini, Radhia Msuya, wabunifu wa mavazi kutoka nchi za
Afrika kama Taibo Bacar kutoka Mozambique, David Tlale kutoka Afrika
Kusini, waandishi wa habari kutoka sehemu mbali mbali za dunia na wadau
wa mitindo.
Mercedes
Benz Fashion Week Africa 2014 ni onyesho la kimataifa linalofanyika
nchini Afrika Kusini mara moja kwa mwaka likikusanya zaidi ya wabunifu
wa mavazi 35 kutoka Afrika kwa ajili ya kuonesha ubunifu wa mavazi yao
ambapo kwa mwaka huu Sheria Ngowi ni mbunifu pekee aliyechaguliwa katika
onyesho hilo kutoka Tanzania.
Sheria
Ngowi anasifika kwa ubunifu wa mavazi aina ya suti, kanzu,sare za
makampuni, mashirika, shule na hafla mbalimbali kama harusi.Mbunifu huyu
alifungua rasmi ofisi zake zilizopo Masaki, mtaa wa Buzwagi mkabala na
Ubalozi wa Angola mwaka mmoja na nusu uliopita ambapo alianza kazi kwa
kuwatengenezea mavazi watu kutoka nchi mbalimbali duniani.
Pongezi nyingi kwa Sheria Ngowi, unaipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa kipaji chako na kazi zako nzuri.
Post a Comment