WAZIRI Mkuu wa zamani Edward Lowassa, amechukua fomu kupeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimpitishe kugombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ifikapo Oktoba 25 mwaka huu.
Katika Makao Makuu ya chama chake hicho kipya leo Edward Lowassa alipokewa na maelfu ya watu waliovalia sare za chama huku wakiimba wana imani naye.
Edward Lowassa aliwasili makao makuu mchana moja kwa moja akaenda ofisi za Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa.
Huku akisindikizwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, Mwanasheria wa chama Tundu Lissu na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Edward Lowassa aliingia katika ofisi hizo katika jukwaa maalumu la kupokea fomu.
Lissu ndiye alikuwa mzungumzaji wa kwanza kwa kuwahakikishia wanachama hawakubahatisha kumpokea Lowassa kwa sababu walifanya utafiti wa kina.
“Kamati Kuu imejiridhisha kwa kushirikiana na viongozi wote wa juu akiwemo Katibu Mkuu na manaibu wake wote wawili, Mwenyekiti na makamu wote wawili, wajumbe wa Kamati Kuu na Mkutano Mkuu, kuwa Edward Lowassa ndiye kiongozi tunayemtaka hivyo Jumapili iliyopita tuliitisha Kamati Kuu ya dharura kumpitisha,” alisema Lissu.
Baada ya kukabidhiwa fomu aliyolipiwa na wanachama waliochangishana fedha hadi kufikia Sh milioni moja, Edward Lowassa alisimama kuwasalimia waliohudhuria kwa kuwaahidi kufanya kazi kwa juhudi ili kuiondoa Tanzania katika hali mbaya ya kiuchumi.
“Nashukuru kwa kunipa heshima kubwa namna hii, sina maneno ya kuwashukuru zaidi ya kuahidi kufanya kazi kwa bidii ili iwe malipo ya mlichonifanyia.
“Shukurani yangu itakuja baada ya kushinda uchaguzi, lakini ushindi hauji bila umoja. Chadema inaweza kuleta mabadiliko kupitia ukawa.
Baada ya kumaliza kuzungumza alisimama Mbowe kutoa neno la shukurani kwa Edward Lowassa kwa kusema Chadema kitaendelea kuwa chama makini kinachosimamia maamuzi yake.
Vilevile alizungumzia ratiba ya vikao vya kujadili fomu ya mgombea ambaye mpaka sasa ni Edward Lowassa pekee, “Vikao vitaanza Agosti mbili kujadili namna tutakavyoingia katika uchaguzi mkuu.
“Baraza Kuu litaketi Agosti tatu kujadili fomu ya mgombea na kujadili ilani ya uchaguzi, Mkutano Mkuu utafanyika Agosti nne kupitisha jina la mgombea na mgombea mwenza.
“Vikao vya kamati Kuu vitaendelea tarehe tano, sita hadi saba kuidhinisha wagombea wa ubunge kwa kushirikiana na Ukawa. Kazi ya kujadili wagombea si ndogo nawaomba waandishi wa habari muwe wavumilivu msipige ramli,” alisema Mbowe.
Baada ya kumalizika hafla hiyo Edward Lowassa alitoka nje kwa ajili ya picha ya pamoja kuwaonyesha wanachama fomu yake.
Post a Comment