Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akipokea TUZO maalum ya “ CWL International Women of Excellency Award for Leadership” kutoka kwa Profesa Joseph Adaikalam, Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Chuo Kukuu cha Binary kilichoko nchini Malaysia kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika maendeleo ya wanawake nchini Tanzania na Afrika tarehe 24.7.2015. Aliyesimama (kushoto) ni Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Dkt. Aziz Mlima, akifuatiwa na Profesa Bulochana Nair na Kulia ni Profesa Datin Rohini Devi wa Chuo Kikuu cha Binary.
PICHA NA JOHN LUKUWI.
……………………………………………………………………………………………….
Na Anna Nkinda – Kuala Lumpur, Malaysia
Mke wa Rais Mhe. Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya mwaka 2015 ya Kiongozi bora Mwanamke (International Woman of Excellence Award for Leadership) na kituo cha Uongozi cha wanawake cha chuo kikuu cha Binary cha nchini Malaysia kutokana na mchango wake mkubwa katika uhamasishaji wa maendeleo ya wanawake watanzania.
Tuzo hiyo imetolewa leo na Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa chuo hicho Prof. Joseph Adaikalam katika ukumbi wa mikutano uliopo chuo kikuu cha Binary kilichopo Kuala Lumpur nchini Malaysia.
Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mhe. Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alikishukuru kituo hicho na kusema amefarijika kwa kuona jinsi kinavyothamini maendeleo ya Wanawake wa Afrika na Dunia kwa ujumla. Kwa kupitia tuzo hiyo wameonesha jinsi wanavyotambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na wanawake.
Mhe. Mama Kikwete alisema “Tuzo hii siyo yangu pake yangu bali ni ya ushindi wa wanawake wote wa Tanzania, Afrika na maeneo mengine ambao wanafanya jitihada kubwa ya kukabiliana na vikwazo kadhaa vinavyowazuia kupiga hatua kubwa ya maendeleo. Mafanikio yanayoonekana yanapatikana ingawaje safari bado ni ndefu na yenye changamoto nyingi”.
Nilipoanza majukumu yangu kama Mke wa Rais wa nchi yetu, nilitambua umuhimu wa kuwa na chombo kitakachoniwezesha kuhamasisha jamii na rasilimali ili niweze kutoa mchango wangu kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu. Hivyo nilianzisha Taasisi ya WAMA ikiwa na Dira ya kuiona Tanzania ambayo wanawake wanawezeshwa na kuishi maisha bora”.
Aliendelea kufafanua kwamba tangu awali alitambua ili kumkomboa mwanamke ni muhimu kuzingatia mazingira na mahitaji yake yote kwa pamoja. Alitambua kwa kumpatia mtoto wa kike elimu, kutamuepusha na ndoa za utotoni, ujauzito katika umri mdogo, kutapunguza matukio ya vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto wachanga.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alimalizia kwa kusema kuwa mwanamke aliyeelimika anatambua na kuweza kutumia fursa za kiuchumi na kujiendeleza yeye mwenyewe na jamii inayomzunguka.
Akisoma wasifu wa Mhe. Mama Kikwete Prof. Sulochana Nair ambaye ni Makamu na Mtendaji Mkuu wa Chuo hicho alisema tuzo hiyo ni ya juu na kwa mara ya kwanza imetolewa kwa mke wa Rais hii ni kutokana na kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake, watoto na watanzania kwa ujumla.
Prof. Sulochana alisema Mama Kikwete kupitia Taasisi ya Wama ametoa fursa za elimu ya sekondari kwa watoto wa kike ambao ni yatima na wengine wanaotoka familia masikini hadi sasa zaidi ya watoto 800 wamenufaika, kufanya uraghibishi dhidi ya ndoa za utotoni, mimba katika umri mdogo.
Kupiga vita maambukizi ya VVU kwa vijana na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ,kufanya uraghibishi ili kuishirikisha jamii katika kutoa chanjo, upimaji na matibabu ya saratani za shingo ya kizazi na matiti, kutoa mafunzo na uratibu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Tuzo ya kimataifa ya Kiongozi bora Mwanamke (International Woman of Excellence Award for Leadership)inayotolewa na kituo hicho pale wanapoona na kutambua mchango wa mwanamke aliyejitokeza kwa juhudi zake za kusaidia na kuhamasisha maendeleo ya wasichana na wanawake Duniani.
Post a Comment