MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TANZANIA (PTA), YATOA SHILINGI MILIONI MBILI KUSAIDIA WANAHABARI WANAOPAMBANA NA UJANGILI NCHINI

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (PTA), Awadh Massawe akizungumza na wanahabari wakati akikabidhi hundi ya sh.milioni mbili kwa Taasisi ya Habari Development Association Dar es Salaam jana asubuhi. 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (PTA), Awadh Massawe (kushoto), akikabidhi mfano wa hundi ya sh.milioni mbili kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Habari Development Association (HDA), Kunze Mswanyama (kulia), Dar es Salaam jana asubuhi kwa ajili ya kuandaa mafunzo ya kuwawezesha waandishi wa habari kujenga weledi wa kufanya tafiti na kuandika habari za kupambana na ujangili. Wa pili kushoto ni Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa TPA, Focus Mauki na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Benard James.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Habari Development Association (HDA), Kunze Mswanyama (kulia), akizungumzia kuhusu mafunzo na umuhimu wa wanahabari katika kupambana na ujangili wa rasilimali za taifa kabla ya kukabidhiwa msaada wa sh.milioni 2 kutoka PTA. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa PTA, Awadh Massawe.


Kaimu Mkurugenzi wa PTA, Awadhi Massawe (katikati), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Kushoto ni Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa TPA, Focus Mauki na Mkurugenzi wa Taasisi ya Habari Development Association (HDA), Kunze Mswanyama.

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imetoa sh. milioni 2 kwa Taasisi ya Habari Development Association kwa ajili kuandaa mafunzo ya kuwawezesha waandishi wa habari kujenga weledi wa kufanya tafiti na kuandika habari za kupambana na ujangili.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe alikabidhi hundi ya thamani ya fedha hizo kwa Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Kunze Mswanyama jijini Dar es Salaam jana.“Tunaunga mkono juhudi hizi za kupambana na ujangili,” alisema Massawe. 

Alisema TPA imefanya hivyo kwa kuwa nchi ina tatizo la uwindaji haramu hasa wa ndovu na usafirishaji wa pembe za ndovu na kulisababishia hasara taifa kupitia mipaka yake.

Alifafanua kuwa bandari ya Dar es Salaam ni sehemu ya mpaka wa taifa, hivyo lazima TPA iunge mkono juhudi za kuelimisha jamii na kuzuia uhalifu huo.

Massawe alisema kwa sasa wanatarajia kufunga kamera 400 za CCTV ili kuimarisha ulinzi na kuwa skana tatu zimeletwa bandarini kwa ajili yakuziongezea nguvu skana mbili zilizopo.

Pia, alisema wanatarajia kupata msaada wa mbwa maalumu wa ulinzi watakaotolewa na Serikali ya Marekani. Alisema TPA inaendelea kuwajengea uwezo wafanyakazi kimaadili ili kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uaminifu kwa faida ya taifa.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Mswanyama alisema fedha walizopewa watazitumia kwa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari 54  kwa masuala ya ujangili kupata weledi na kutafiti na kufichua ujangili. “Tunahitaji kujenga uwezo wa kupambana na ujangili  ili taifa liweze kunufaika nazo,” alisema. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)




Post a Comment

Previous Post Next Post