Na Andrew Chale, Modewjiblog
Bendi mpya ya muziki wa dansi ijulikanayo kama The Stars Band iliyo chini ya Anneth Kushaba inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumamosi ya Julai 18, siku ya Idd-Mosi ndani ya kiota cha Mzalendo Pub, Kijitonyama jijini Dar es Salaam huku ikitarajiwa kusindikizwa na mwanamuziki Barnabas pamoja na bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’
Kiongozi wa Stars Band, Kushaba anasema kuwa, tayari wapo katika mazoezi mbalimbali na ‘crew’ nzima ya bendi hiyo ambayo inaunganisha wanamuziki wenye uzoefu mkubwa katika uimbaji, upigaji vifaa na kushambulia jukwaa ndani na nje ya Tanzania.
“Wadau wa burudani ni nafasi ya kipekee kujitokeza kushuhudia uzinduzi wa bendi yao mpya iliyojaa kila aina ya burudani kuanzia uimbaji, kumiliki jukwaa na vyombo vilivyopangika burudani itakayoanza kuanzia saa moja jioni hadi majogoo” anasema Kushaba.
Anaongeza kuwa, uzinduzi huo pia utapambwa na bendi ya Fm Academia ‘Wazee wa NGWASUMA na mwanamuziki Barnabas Classic huku kiingilio mlangoni kitakuwa sh 10,000.
Kushaba anasema kuwa, miongoni mwa wanaounda bendi hiyo wapo wakali katika upande wa uimbaji kama Mao Santiago, Felly Kano, Alawy Junior, Khajanito (Khadija Maumivu) na Aneth Kushaba.
Kwa upande wa vyombo bendi hiyo inaundwa na mpiga drum wa zamani wa Twanga Pepeta, James Kibosho akiwa pamoja na Zaid Sato (Base), Othuman Majuto, Sebastian na Denis ‘Keyboard’, pamoja na Chacha ‘Tumba’.
Stars Band ndio inakuwa bendi ya kwanza ya dansi nchini kuja na mitindo mipya ya Utamaduni na bongo fleva (None stop!!) jukwaani.
Stars Band pia baada ya uzinduzi huo itakuwa inapiga kila Jumamosi ndani ya kiota hicho cha Mzalendo Pub.
Post a Comment