TAARIFA YA MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU

Serikali kupitia Wizara yangu inaendelea na utaratibu wa kutoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini kila wiki kama tulivyoahidi. Takwimu za ugonjwa huu zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 22 Mei 2016, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 21,585  ambao wametolewa taarifa ya kuwa na ugonjwa huu, na kati ya hao, ndugu zetu 338 wamepoteza maisha.
Tumefarijika kuona takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei 2016 zinazoonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imepungua kwa asilimia 49 (karibu nusu ya wagonjwa), ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa ni 108, na hakuna aliyepoteza maisha, ikilinganishwa na wagonjwa wapya 212 walioripotiwa wiki iliyotangulia ya Mei 9 hadi 15.
Mikoa ambayo imeripoti wagonjwa wiki hii ni Morogoro (47), Manyara(16), Lindi (14), Mara (11) Dar es Salaam (9), Pwani (6), Kagera (2), Kilimanjaro (2) na Iringa (1).
Halmashauri zilizoongoza kutoa wagonjwa wengi ni Kilosa (27),  Mvomero (15), Kilwa (14), Tarime Mjini (11), Babati Vijijini (10), Kinondoni (9), Babati Mjini (5), Morogoro Mjini (5), Kibaha Mjini (4), Bukoba Mjini (2), Chalinze (2), Same (2), Iringa Mjini (1) na Mbulu (1).
Katika wiki iliyopita, mikoa ambayo haikuwa na wagonjwa wa kipindupindu ni Kigoma, Dodoma, Mwanza, Geita, Singida, Shinyanga, Arusha, Tanga, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Simiyu na Mtwara. Na mikoa ambayo haijawahi kuripoti mgonjwa wa kipindupindu tangu mlipuko uanze ni Ruvuma na Njombe
Kupungua kwa idadi ya wagonjwa kusirudishe nyuma juhudi za kuuzuia ugonjwa huu, bali tunatakiwa kuzidisha jitihada ili tuweze kuuondoa, tusiwe na wagonjwa kabisa. Ni vema kuchukua tahadhari zaidi, hasa katika msimu wa masika, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa maji ya mvua kusambaza vimelea vya ugonjwa huu. Tuendelee kuzuia maambukizi, na pia kuendelea kutoa taarifa za ugonjwa kila siku, hata kama hakuna wagonjwa, na kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huo
Wizara inaendelea kutoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira. Aidha Wizara inatoa elimu ya afya kwa njia ya kupiga simu kupitia namba 117 na kwa njia ya kutuma ujumbe wenye neno KIPINDUPINDU kwenda 15774. Huduma hizi zinatolewa bila malipo kupitia mitandao yote.
Napenda kusisitiza tena kwamba ni   marufuku   kwa   watu   kutitirisha   maji   taka   ovyo, hasa katika kipindi hiki cha mvua na  mamlaka husika zinatakiwa kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote watakaokiuka agizo hili. Aidha tunawasihi viongozi mbalimbali wa ngazi zote; za vitongoji, vijiji, kata na tarafa kusimamia kikamilifu suala hili. Wizara inasisitiza kwamba kila jitihada zifanyike kote nchini ili kuhakikisha kuwa jamii yote ya Watanzania inatumia maji safi na salama. Hii ni pamoja na kuzingatia taratibu za kutibu maji ya kunywa katika ngazi ya kaya.
Tunaendelea kuisihi jamii kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
  • Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunamoishi ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu.
  • Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
  • Mamlaka za maji zihakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
  • Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu,
  • Kuhakikisha maji ya kunywa yanachemshwa au kutibiwa kwa dawa. Na hapa napenda kusisitiza kwa wananchi wanaokaa kandokando ya Mto Pangani, kuwa maji ya mto huo si salama, yameingia vimelea vya kipindupindu na kumetokea wagonjwa wengi katika eneo hilo. Ni muhimu sana kuyachemsha au kuyatibu kwa dawa maji hayo kabla ya kuyatumia nyumbani.
  • Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
  • Kuzingatia matumizi sahihi ya ORS kwa wagonjwa walioanza kuonesha dalili ili kupunguza athari za ugonjwa.
  • Watumishi wa afya kutoa takwimu sahihi na kamili za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika juhudi za kutokomeza kipindupindu. Aidha, inawapongeza na kuwashukuru wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa na katika kusimamia kikamilifu  miongozo inayotolewa na Wizara ili kuutokomeza ugonjwa huu, wakiwemo wataalamu wa sekta mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post