MKUU WA MKOA WA RUKWA ATOA AMRI KUHUSU KUPOKEA, KUINGIZA, KUIHAMISHA, KUSAFIRISHA NA KUPITISHA MIFUGO NDANI YA MKOA WA RUKWA

Mkuu wa mko wa Rukwa kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewaagiza wakuu wa Wilaya kutokubali kupokea mifugo kutoka katika wilaya nyingine bila ya mifugo hiyo kuipa kibali maalum cha kuhamia katika wilaya zao.
Ameyasema hayo katika amri halali namba 1/2017 kuhusu kupokea, kuingiza, kuihamisha, kusafirisha na kupitisha mifugo ndani ya mkoa wa rukwa kwa mamlaka aliyopewa na kifungu cha 7 cha sheria Nambari 19 ya mwaka 1997 ya Tawala za Mikoa Sura Namba 97 mapitio ya mwaka 2002, kwa lengo la kusimamia na kutekeleza maagizo ya waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2002 unaokataza kabisa usafirihaji kiholela wa mifugo.
“Mifugo isihamishwe kutoka katika Kijiji, Wilaya ama Mkoa kabla ya kupata kibali cha Kijiji, Wilaya ama Mkoa inakopelekwa. Hivyo Kijiji, Wilaya na Mkoa itatoa kwanza idhini ya kupokea mifugo hiyo ndipo kibali cha kusafirisha mifugo kitolewe,” Zelote Stephen alisema.
Zelote Stephen alisisitiza kuwa Vijiji, Wilaya na Mkoa usitoe vibali vya kupokea mifugo kabla ya kujiridhisha kwamba wanayo maeneo ya kutosha ya malisho ya mifugo, yaliyopimwa na kuthibitishwa na wataalamu kama yanafaa kwa malisho na maji ya kutosha na majosho ya kuoshea mifugo.
Vile vile Mkuu wa Mkoa aliwaagiga maafisa mifugo kuanzia ngazi ya Kijiji, Wilaya na Mkoa kusisimamia na kuhakikisha hakuna mifugo inayosafirishwa kutoka Kijiji, Wilaya na Mkoa kwenda Mkoa mwingine au kuingia katika Kijiji, Wilaya au Mkoa bila ya kupimwa na kuchanjwa chanjo lengo likiwa ni kuthibiti uenezaji wa magonjwa ya mifugo nchini.
“Kabla ya kutoa vibali vya kusafirisha mifugo, madaktari wa mifugo wa Wilaya ama wawakilishi wao wahakikishe kwamba mifugo inaogeshwa na kuchanjwa dawa za kuzuia magonjwa husika kabla ya kuiruhusu mifugo hiyo kusafirishwa ili kuzuia uenezaji wa magonjwa ya mifugo,” Zelote Stephen alifafanua.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewatahadharisha maafisa mifugo ambao sio waaminifu wanaotumia njia ya kuingiza mifugo kwenye wilaya kwa njia ya biashara za minada na matokeo yake mifugo hiyo kubaki eneo husika bila ya kufuata taratibu zozote.
Amri hii itafanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 9 January, 2017 hadi tarehe 31 Desemba, 2017.

Post a Comment

Previous Post Next Post