WASICHANA 8000 KUNUFAIKA NA MRADI WA UNESCO WA ELIMU
www.habarika24.blogspots.com0
Wasichana 8,000 waliopo shuleni na 600 ambao hawako shuleni watanufaika na mradi mkubwa wa kuwawezesha wasichana na wanawake vijana kupata elimu.
Mradi huo wa miaka minne wenye gharama ya dola za Marekani milioni 5 utafanyika katika wilaya tano nchini.
Wilaya hizo ni Ngorongoro, Kasulu, Sengerema, Micheweni na Mkoani.
Mradi huo ambao upo hatua ya pili umeanza kwa kongamano lililofunguliwa jana na Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo.
Mradi huo mkubwa kwa mujibu wa Katibu mkuu huyo umelenga kuwaokoa wanafunzi kabla hawajakumbwa na matatizo yanayokatisha masomo yao.
Aidha utawapa fursa za kuboresha zaidi mafunzo mbalimbali waliyonayo ambao utawafanya kuwa watu wazuri zaidi katika jamii na hivyo kuchangia maendeleo ya taifa na jamii walizopo.
Katibu mkuu huyo ambaye alifungua kongamano na kuzindua mradi huoi awamu ya pili alisema kwamba ni matumaini yake kwamba jamii itaukumbatia mradi huo ili kuwa na taifa lenye mafanikio makubwa katika malengo ya maendeleo endelevu ya dunia kwa kuzingatia lengo namba tano.
Amewataka wazazi na vijana kutimiza wajibu wao kwa kubadilika kitabia na kutambua umuhimu wa elimu katika kufanikisha wanachotaka ambacho ni maendeleo binafsi , familia na taifa kwa ujumla.
Katika hotuba yake alisema ni matumaini kwamba wadau katika mradi huo watafaikisha katika kipindi cha miaka minne mipango yote iliyolenga kuboresha huduma kwa wasichana na wanawake vijana, kushawishi jamii kubadilika na kuachana na tamaduni mbaya kama ndoa za utotoni na ukeketaji.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na utamaduni UNESCO, Zulmira Rodrigues alisema mradi huo ulioanza mwaka jana na kufanyiwa tathmini umeonesha changamoto kubwa ya watoto wa kike ikiwamo mimba za utotoni,ukeketaji na kushindwa masomo.
Alisema lengo la mradi ni kuhakikisha kwamba mwanamke anapata fursa za kupambana katika mazingira yake kama anavyofanya mwanaume kwa kuwezeshwa na kuzuia mila, tabia na tamaduniu mbaya ambazo zinakwamisha uwezo wake wa kuhudhuria masomo.
Aidha alisema mradi huo utatoa nafasi kwa wanawake vijana ambao wamekosa masomo au wameacha masomo au hawakwenda shule kabisa kupata nafasi ya kusoma.
Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la kimataifa la misaada la Korea (KOICA) kupitia UNESCO na kufanyiwa kazi pia na mashirika ya UN Women na UNFPA unaangalia namna bora ya kukabiliana na changamoto za mabinti wanaokwenda shule katika wilaya hizo ili kuwawezesha kuwa watu bora katika jamii siku za usoni.
Post a Comment