CHANGAMOTO YA UPATAJI WA MAJI YA KUTUMIA NI TATIZO LA ZAIDI YA MIAKA 30 MPAKA SASA.


Na. Frank Bunini- Dodoma
Bi Aisha Abdallah (37), mkazi wa kijiji cha Madaha, Wilaya ya Chemba, Mkoani Dodoma alivunjika mkono baada ya kuanguka na Baiskeli akiwa anatoka Kisimani kuchota maji yakutumia nyumbani kwake.

Baiskeli ilimlalia baada ya kupoteza uelekeo njiani kutokana na ubovu wa barabara. Watu wanalazimika kutumia Baisikeli  kwenda kubebea maji  Kisimani kutokana na Kisima kua mbali sana na makazi yao, kutoka yalipo makazi mpaka kufika kwenye Kisima wanacho chota maji ni  urefu wa kilomita 4 (kutoka nyumbani hadi kisimani). 

Amesema kuwa baada ya kuanguka na Baisekeli, kuna mama wanaeishi nae kijiji kimoja alikua anapita ndio alimuona akiwa amelaliwa na Baiskeli akibidi mama huyo amsaidie kumyanyanyua pale chini akiwa amesha vunjika mkono; wakiwa wako eneo lile la tukio ilitokea Trekta ikitoka shambani, wakaisimamisha na kumuomba dereva wa Trekta msaada wa kuwabeba.

 

"Nilipelekwa na Trekta nyumbani kwangu nikiwa na mwanamke mwenzangu ambaye alinipatia msaada wa kuninyanyua wakati nimeanguka na Baiskeli nikiwa natoka kuchota maji Kisimani, Trekta hilo lilikuwa linatoka shambani na dereva wake alinikuta nipo njiani na mwenzangu hivyo alitubeba na kutupeleka haraka nyumbani".

"Naiomba Serikali yetu ya Mama Samia itusaidie kututatulia changamoto ya maji hapa kijijini kwetu kwasababu akina mama inatuathiri sana hii hali, kwasasa nasaidiwa na mama yangu pamoja na binti yangu wa darasa la kwanza ambaye ananichotea maji kabla hajaenda shule". Alisema Bi Aisha Abdallah.       Akina mama wa kijiji cha Madaha wilaya ya Chemba wakiwa kisimani wakichoto maji.              Mama mzazi wa Bi. Aisha Abdallah.

Aidha pia Mama Mzazi wa Bi Aisha Abdallah, Bi Mwanaidi Ramadhani, amesema kuwa alipelekewa taarifa na watoto  wakati yeye akiwa porini kutafuta kuni;  ilimlazimu kurudi nyumbani haraka  na kumpatia huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka kwa mtaalamu kwa ajili ya matibabu zaidi.


Bi Mwanaidi ameiomba serikali kuwasogezea wakazi wa kijiji hicho huduma ya maji safi na salama karibu na mazingira yao ili kupunguza kadhia kama hizi katika kijiji hicho.


"Tunaiomba serikali itutatulie changamoto za maji, wananchi inatulazimu kwenda usiku wa manane kisimani, kutokana na upatikanaji wa maji kua ni shida kule kisimani na ukizingatia maeneo hayo kuna wanyama wakali kama fisi, inakuwa ni hatari kwetu kama wanawake" Alisema Mama mzazi wa Aisha, Bi Mwanaidi Ramadhani.            Mwenyekiti wa Kitongoji Bw. Majidi Hassani

Mwenyekiti wa Kitongoji Bw. Majidi Hassani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo familia hiyo ilimtafuta kumpatia taarifa hizo na kushirikiana nao kwa ajili ya matibabu ya Bi Aisha.

Pia amesema kuwa kutembea umbali mrefu kufata huduma ya maji kunachangia kwa kiasi kikubwa watu kuanguka kutokana na uchovu huku ikiwagharimu katika shughuli nyingine za kiuchumi.


"Kwa niaba ya wananchi wangu naiomba serikali kuu itusikie kilio chetu wananchi wa kitongoji cha Malari, maji yamekuwa ni changamoto ambayo inatupa shida hata kwa watoto wetu wanaosoma sio tu akina mama peke yao".


"Watoto wanaweza kwenda shule hawajafua nguo, akina mama wanaweza pia kuacha watoto nyumbani muda mrefu kwasababu ya kutafuta maji, tunaomba serikali ituchimbie visima ambavyo vitatupa maji safi na salama" Alisema Mwenyekiti wa Kitongoji cha Malari, Bw. Majidi Hassani.


Bi Aisha Abdallah kwasasa ni mjane na ana watoto nane (8), kwa sasa anasaidiwa na mama yake mzazi pamoja na mtoto wake wa darasa la kwanza. Changamoto ya maji ipo kwa takribani miaka 30 kijijini hapo.  Ambapo maji yaliyopo ni umbali wa zaidi ya kilometa 2 kutoka kwenye makazi na pia  sio maji safi na salama kama ambavyo inahitajika kwa matumizi ya binadamu.           Picha na Abutwalibu Mustafa wa Habarika24.

    Kwa habari za kijamii, habari za utalii, habari za Watoto, na habari za kuelimisha, wasiliana                                                         na Habarika24 kupitia +255 784747478 


Post a Comment

Previous Post Next Post