SERIKALI YATOA LESENI KUBWA YA UCHIMBAJI MADINI NA USAFISHAJI MADINI

-Ni kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Ltd-(Pangani)na Tembo Nickel Corporation Ltd(Kahama)

-Waziri Mavunde ataka fidia kwa wananchi wa Pangani ilipwe kwa wakati

-Aagiza Mradi kutoathiri shughuli za kawaida za wananchi za uvuvi

-Kampuni ya Tembo Nickel kuwekeza dola Milioni 500 kiwanda cha usafishaji madini

-Bidhaa ya kutengeneza betri ya magari ya umeme kuzalishwa Kahama

Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde leo ameshuhudia makabidhiano ya   Leseni ya Uchimbaji Mkubwa Madini ya Mchanga Mzito wa Bahari (heavy mineral sands) kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited na leseni ya kiwanda cha uchenjuaji wa madini ya metali (multi-metal refinery) kwa Kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited.


- MRADI WA TAJIRI-WILAYA YA PANGANI,TANGA.

Jumla ya kiasi cha dola za Marekani milioni 127.7 zitawekezwa katika mradi huu, ambapo Serikali itakusanya  mapato takribani dola za Marekani milioni 437.96 kutokana na gawio la hisa za Serikali, kodi na tozo mbalimbali; Ajira za watanzania,kuongezeka kwa fursa za biashara; na kuimarika kwa hali ya kiuchumi na ustawi wa jamii kutokana na uwepo wa miradi ya huduma za jamii zitakazotolewa kupitia utaratibu wa Corporate Social Responsibility (CSR).

Uchenjuaji wa makinikia ya heavy mineral sands utazalisha madini kama zircon, leucoxene, rutile, garnet monazite na ilmenite. Madini ya Heavy Mineral Sands hutumika kutengeneza mapambo, vifaa tiba, vifaa vya nyuklia, injini za ndege, saa, simu, kompyuta mpakato (laptop) na vyungu vya kuyeyushia metali (crucibles). Soko kubwa la madini hayo kwa sasa ni katika nchi za Marekani, China, Japani, Korea, India na Afrika Kusini.


-KIWANDA CHA USAFISHAJI MADINI-KAHAMA,SHINYANGA.

Kiwanda cha usafishaji wa madini ni kiwanda kitakachomilikiwa na kampuni ya Tembo Nickel Refining Limited ambayo ni kampuni tanzu ya kampuni ya ubia ya Tembo Nickel Corporation Limited ambayo inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya LZ Nickel ya Uingereza.

Takribani kiasi cha dola za Marekani milioni 500 zitawekezwa katika kiwanda hicho kitakachotumia teknolojia ya hydrometallurgy ikiwa ni mbadala wa technolojia ya uyeyushaji (smelting) na hivyo kuwa na gharama nafuu za uendeshaji na uzalishaji bora wa metali baada ya uchakataji. Aidha, kwa kupitia teknolojia hiyo makinikia yatakayozalishwa kwa njia ya flotation katika mgodi wa Kabanga na mingine nchini yataweza kuchakatwa na kuzalisha metali zenye ubora wa asilimia 99.9.

Waziri Mavunde ametumia fursa hii kumshukuru Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuweka mazingira mazuri yanayovutia uwekezaji nchini na kupelekea uwekezaji huu mkubwa utakaochochea ukuaji wa sekta ya madini na Uchumi wa Tanzania.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Mh. Constantine Kanyasu amesema kamati ya Bunge itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ili miradi hii ilete manufaa kwa umma.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Wakuu wa mikoa wa Tanga na Shinyanga mtawalia Mh. Dkt. Balozi Batilda Burian na Mh. Annamringi Macha wakiongozana na wakuu wa Wilaya za Pangani na Kahama.

Post a Comment

Previous Post Next Post