Na Magreth Kinabo, Dodoma
26/08/2014.
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu ya Bunge hilo, Dkt. Francis Michael ametoa ufafanuzi kuhusu suala la utungaji wa Katiba ambalo hufanyika kwa mifumo miwili, na kuwataka wananchi wasipotoshwe na mfumo unaotumika.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni mtaalam wa sheria wakati akizungumza katika kipindi cha Jambo kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Akifafanua kukuhusu mifumo hiyo, amema kuwa kuna mfumo wa kwanza ,ambao hutumia Tume kama ilivyokuwa Tume ya Jaji Joseph Warioba yenye watu ambayo ilikuwa na kazi ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na kutengeneza Rasimu ya Katiba Mpya , baadaye Bunge Maalum la Katiba linapitia maoni ya Rasimu hiyo, ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2014 linaweza kubadilisha na kuongeza kwa ajili ya kuiboresha.
“Katika mfumo huu lazima Bunge liwepo kwa ajili ya kuiboresha kabla ya kwenda kupigiwa kura na wananchi,” alisema Dkt. Michael .
Dkt. Michael aliutaja mfumo wa pili ni ule wa kutumia Tume Maalum ya Wataalam, ambao wanawajibu wa kuandika Katiba na hakuna chombo chochote kitakachokuwa na wajibu wa kuibadilisha, bali itakwenda moja kwa moja kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.
“Wananchi wasichanganywe na mfumo unaotumika,” alisisitiza Dkt. Michael.
Akizungumzia kuhusu uwasilishaji wa nyongeza ya mapendekezo yaliyowasilishwa na makundi mbalimbali hivi karibuni kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta yamepokelewa kwa mujibu wa sheria hiyo, kipengele cha 25 ambapo Bunge hilo lina nguvu kufanya marekebisho au kuongoza vifungu vingine pale linapoona inafaa.
Aidha, Dkt. Michael amefafanua kuwa wanatumia nafasi hiyo kisheria na kikanuni, kupokea nyongeza ya mapendekezo hayo kutoka kwa watu mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu suala hilo, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe, Ridhiwani Kikwete alisema linafanyika kisheria hivyo mtu au kikundi kinaweza kuwasilisha mapendekezo ya nyongeza.
Mhe, Ridhiwani alisema nyongeza ya mapendekezo hayo, uwasilishwa kwenye Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo, ambayo nayo hupeleka kwa Kamati 12 za Bunge hilo kwa ajili ya kuratibu mambo ya msingi na kuyachukua .
Aliongeza kuwa suala hilo pia linaweza kufanyika wakati wa mjadala wa Bunge hilo,mjumbe anaweza kulishawishi Bunge hilo, kwa kuwa sheria , kanuni na miongozo inaruhusu.
Post a Comment