VYAMA VITANO VYA SIASA VISIVYO NA WABUNGE VYAOMBA SAKATA LA IPTL LIMALIZWE

Dotto Mwaibale 

 MAKATIBU wakuu wa vyama vitano vya kisiasa visivyo na wabunge bungeni wameomba suala la utata wa ufisadi zaidi ya sh.bilioni 300 zilizowekwa katika akaunti ya Tegeta Escrow zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) limalizwe ili kuendelea kwa mambo mengine ya kitaifa.

 Katika hatua nyingine makatibu hao wamepinga hatua ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) kukabidhi ripoti ya uchunguzi kwa Waziri Mkuu na kudai ipelekwe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DDP) mwenye uwezo wa kuchukua hatua za kisheria.

 Makatibu hao ni kutoka Chama cha Kijamii (CCK), Sauti ya Umma (SAU), Union For Multiparty Democracy (UMD), Alliance Farmaers Party na Demokrasia Makini (DM) ambavyo vimetoa tamko hilo Dar es Salaam leo wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata hilo linaloendelea bungeni mjini Dodoma. 

 Tamko la makatibu hao limekuja siku moja tu baada ya kuwepo taarifa kuwa Waziri Mkuu, Pinda atakabidhi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda ripoti ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow kufuatia madai ya uchotwaji wa Dola za Marekani milioni 200 (Sh. bilioni 320). 

 Makatibu wakuu wa vyama hivyo,Renatus Muabhi (CCK), ,Ali Kaniki (SAU), Rashid Rai (AFP),Dominick Lyamchai (Demokrasia Makini)na Kibaya Kiahira (UMD) walisema Takukuru kupeleka ripoti ya uchunguzi wa suala hilo bungeni siyo sahihi kwasababu ina utaratibu wake wa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria. 

 “Kiutaratibu Takukuru wakikamilisha uchunguzi wa jambo lolote inatakiwa kisheria kupeleka ripoti hiyo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP) na baada ya DPP kuipitia atatoa maoni yake ya kisheria kama kuna umuhimu wa kufungua mashtaka,”alisema Ali Kaniki Katibu Mkuu wa chama cha SAU. 

 Kaniki alisema ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ripoti yake ya uchunguzi kujadiliwa bungeni ni sahihi kwasababu utaratibu kama huo umekuwa ukitumika hata katika uchunguzi wa mambo mengine lakini siyo ripoti ya Takukuru. 

 Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama cha CCK,Renatus Muabhi, alisema inashangaza bunge kuendelea kung’ang’ania suala la IPTL wakati halina tija kwa Watanzaia katika kipindi hiki ambacho nchi inakabiliwa na matatizo mengi. 

 “Bunge nalo linatoa hadithi tu,wabunge wanapiga kelele kuhusu sakata la IPTL na hatuoni mwisho wa jambo hili,hospitali hazina dawa,kuna suala la katiba ambalo ni muhimu limefunikwa,nchi inakwenda wapi,”alisema. 

 Muabhi alisema Mkurugenzi wa Takukuru, Edward Hosea anapaswa kuwajibika kutokana na uamuzi wake wa kupeleka ripoti ya uchunguzi wa sakata la IPTL kwa Waziri Mkuu. “Dk.Hosea anapaswa kuwajibika sababu ameshindwa kuzingatia sheria katika suala hili,kwanini apeleke hiyo ripoti kwa Waziri Mkuu wanakati anafahamu fika kuwa Waziri Mkuu hahusiki na masuala ya jinai,”alisema Muabhi. 

 Muabhi alisema danadana inayofanywa na serikali katika jambo hilo ni kutaka kuficha ukweli ili wawe waliotajwa katika ripoti ya CAG na Takukuru wasiweze kuchukuliwa hatua za kisheria. 
 Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi (kulia), akizungumza kwa niaba ya vyama vitano visivyo na wabunge Dar es Salaam leo, wakati akitoa tamko la vyama hivyo kuhusu kumalizwa kwa utata wa ufisadi zaidi ya sh.bilioni 300 zilizowekwa katika akaunti ya Tegeta Escrow  zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kutoa fursa kuendelea kwa mambo mengine ya kitaifa. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini, Dominick Lyamchai na Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Ali Kaniki.
 Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Ali Kaniki (wa pili kushoto), akizungumza katika mkutano huo.
 Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance Farmaers Party,Rashid Rai (kulia), naye alipata fursa ya kuchangia jambo.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
                 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post