STARTIMES YAKABIDHI MSAADA WA CHAKULA SHULE YA MSINGI MAALUMU YA AIRWING JIJINI DAR ES SALAAM

Kutoka kulia ni wafanyakazi wa kampuni ya StarTimes Tanzania, Bi. Elena Liu na Paulina Kaka wakifurahia jambo pamoja na Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Airwing, Kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili, Bw. Issa Mkasa wakati wa kukabidhi msaada wa vyakula na mahitaji mengineyo shuleni hapo. Akishuhudia tukio hilo kulia ni Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bi. Fabiola Malisa.
Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (mwenye hijab) akikabidhi moja ya msaada wa chakula na mahitaji mengineyo kwa wanafunzi wa shule ya msingi Airwing, kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili kwa niaba ya wafanyakazi wa kampuni hiyo. Wakishuhudia tukio hilo kutoka wa pili kushoto ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Airwing, Bi. Fabiola Malisa na Mwalimu wa Kitengo hiko, Bw. Issa Mkasa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Airwing, Bi. Fabiola Malisa (kushoto) akifurahia jambo pamoja na Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (kulia) wakati wa kukabidhi msaada wa vyakula na mahitaji mengineyo kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kitengo maalum cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili shuleni hapo. Akishuhudia tukio hilo katikati ni  Mwalimu wa Kitengo hiko, Bw. Issa Mkasa.
Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (mwenye hijab) akikabidhi moja ya msaada wa chakula na mahitaji mengineyo kwa wanafunzi wa shule ya msingi Airwing, kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili kwa niaba ya wafanyakazi wa kampuni hiyo. Wakijumuika pamoja naye katika tukio hilo wa pili kulia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Airwing, Bi. Fabiola Malisa na wa pili kushoto ni Mwalimu wa Kitengo hiko, Bw. Issa Mkasa.


Na Mwandishi Wetu 

Serikali yaombwa kutilia mkazo kuhakikisha kila shule ya msingi inakuwa na kitengo maalumu cha wanafunzi wenye ulemavu wa viungo mbalimbali ili kuwapatia na wao fursa ya kupata elimu.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Shule ya Msingi ya Airwing, Bi. Fabiola Malisa wakati wa kupokea msaada wa chakula na mahitaji mengineyo kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni ya StarTimes Tanzania kwa ajili ya kitengo maalumu cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili.

Bi. Malisa alisema kuwa shuleni kwake wanacho kitengo cha kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili ambao kwa sasa wapo jumla ya 65, wanafunzi 20 ni wasichana na wanafunzi 45 ni wavulana.

“Hapa kitengo maalumu cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili ukiachana na wanafunzi wengine wa kawaida. Kwa sasa tunalo darasa moja ambalo tunawafundishia kwa kupeana amu na wanafunzi wa darasa la pili. Yaani wao wanaingia asubuhi na kutoka saa tano baada ya hapo wanafunzi wengine hulitumia hilo darasa. Tumeamua kufanya hivi kutokana na uhaba wa madarasa wenyewe.” Alisema Bi. Malisa

“Kuanzishwa kwa kitengo hiki lengo ni kuwafundisha watoto hawa wenye ulemavu wa akili nao waweze kupata stadi mbalimbali za kujumuika pamoja na jamii inayowazunguka. 

Jamii hudhani kuwa motto akizaliwa na ulemavu wa aina yeyote ile anakuwa ni mtu tegemezi. Sisi tunakanusha suala hilo kwani tunao hapa ambao tunawafundisha na wengi wameonyesha maendeleo mazuri. Kwa mfano kuna ambao baada ya kumaliza vipindi darasani hurudi wenyewe majumbani na hata kuja wenyewe shuleni kila siku.” Alisema na kuongezea Bi. Malisa

“Sisi kama uongozi wa shule tunajitahidi kadiri ya uwezo wetu kuwasaidia watoto hawa ili wajitambue na kuweza kuishi na jamii. Na tumefanikiwa kwa hilo, kwa mfano tunao wanafunzi wawili ambao baada ya kufundishwa kwenye kitengo hiki na kuonyesha maendeleo mazuri wamejiunga na wanafunzi wa kawaida, mmoja yuko darasa la saba na mwengine la nne,” alisema na kuongezea Mwalimu Mkuu, “Na tena wanasoma bila shida yoyote na wanafunzi wengine wamewazoea wanasoma pamoja nao.”

“Changamoto kubwa tunayokumbana nayo nib ado tuna uhaba wa madarasa kama nilivyoelezea awali tunatumia darasa kwa awamu. Kwani wao wanahitaji muda zaidi tofauti na wanafunzi wa kawaida. Japokuwa tunapokea msaada kutoka serikalini, kwa makampuni na taasisi zingine bado hautoshi. Tunaomba serikali itilie mkazo zaidi kwa kila shule kuwepo na kitengo cha namna hii kwani hali hiyo itapelekea wazazi kutowaficha watoto majumbani. Pia vituo hivi huwapunguzia wazazi mzigo mkubwa wa kuwalea kwani huwa salama mahali hapa na kuwafanya wao kufanya shughuli zingine za kujenga taifa.” Alihitimisha Bi. Malisa

Naye kwa upande wake akiongea kwa niaba ya wafanyakazi, Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif amesema kuwa wao kama kama kampuni na watanzania wameguswa sana na ustawai watoto hawa ambao jamii huwachukilia tofauti.

“Bado watanzania tunayosafari ndefu ya kubadili mtazamo juu ya watoto wenye ulemavu. Tunatakiwa kuondoa dhana ya bado kufikiria ukiwa na motto mlevu basi atakuwa tegemezi kwa maisha yake yote duniani. Ulemavu unatofautiana na ule ambao unaweza kutibika watoto hawa wasaidiwe. Lakini jambo hili halitowezekana kama serikali haitojenga vituo hivi kwenye kila shule ya msingi na pia wadau nao kujitokeza kuziunga mkono.” Alisema Bi. Hanif

“Na kusema ukweli mahitaji ambayo yanahitajika katika shule hizi yamo ndani ya uwezo wetu watanzania. Bado tunahitaji mwamko wa kutosha kwani si wazazi wote wanao uwezo wa kumudu gharama za kuwahudumia watoto wenye ulemavu. 

Tumekuja hapa tumezungumza na walimu wametupa hali halisi kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi hawa uwezo wao ni mdogo hivyo wanahitaji misaada yetu,” alisema na kumalizia Bi. Hanif, “Hivyo basi kwa msaada wetu huu ambao sisi wafanyakazi wa StarTimes tumejikusanya na kuutoa, tunatarajia pia makampuni na taasisi nyingine wataiga na kufanya hivyo. Ni jukumu letu sote kuwasaidia na kuwalea watoto hawa kwani Mungu ana makusudio yake kuwaumba hivi.”


Msaada wa wafanyakazi wa StarTimes Tanzania uliotolea kwa kitengo hiko cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili shuleni Airwing ni pamoja na sukari, mikate, majani ya chai, blueband, chumvi, sabuni za unga na mche, vibiriti, na mengineyo. Msaada huo umelenga kuwahudumia wanafunzi hao kwa muda ambao wapo shuleni na kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)

Post a Comment

Previous Post Next Post