TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA MALAWI.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilikutana na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Januari, 2017 kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma kuhusu Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi ambao umepangwa kufanyika mjini Lilongwe, Malawi tarehe 03 hadi 05 Febuari 2017.
Hata hivyo, vyombo vingi vya habari hususan Magazeti ya tarehe 27 Januari, 2017 vimeandika kwamba Mkutano huo ni maalum kwa ajili ya kujadili mgogoro wa Mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa pamoja na kesi ya Watanzania nane waliokamatwa kwa madai ya kuingia nchini Malawi bila kibali.
Wizara inapenda kuchukua nafasi hii kutoa ufafanuzi kwamba, suala la mgogoro wa mpaka limekwishatolewa taarifa na Wizara hivi karibuni kwamba lipo chini ya Jopo la Usuluhishi linaloundwa na Viongozi Wastaafu wa Afrika kutoka nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC). Jopo hilo linaongozwa na Mhe. Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji akisaidiwa na Mhe. Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana na Mhe. Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini.
Aidha, kuhusu suala la Watanzania nane waliokamatwa kwa madai ya kuingia nchini Malawi bila kibali lipo Mahakamani hivyo halitakuwa sehemu ya mazungumzo ya Mkutano wa Tume ya Pamoja.
Pia, Wizara inapenda kuujulisha umma kuwa licha ya kuwepo kwa mgogoro wa mpaka wa Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, mahusiano ya nchi hizi mbili yamezidi kuimarika siku hadi siku katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hata wananchi wa pande zote mbili za Ziwa wameendelea kuishi kwa amani na ushirikiano wa karibu.
Kwa mantiki hiyo,  Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati  Tanzania na Malawi ni njia mojawapo ya kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili. Mkutano huu ambao ni wa kawaida, una lengo la kujadili na kutathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Tatu wa JPCC uliofanyika Tanzania, tarehe 24 hadi 30 Juni, 2003.
Aidha, mkutano huu utawaleta pamoja watalaam wa nchi hizi mbili kutoka Sekta mbalimbali kwa lengo la kujadili changamoto za ushirikiano katika sekta hizo, kubaini maeneo mapya ya ushirikiano pamoja na kuweka mikakati ya kutekeleza miradi ya pamoja itakayokubaliwa baina ya pande hizi mbili. Masuala mbalimbali ya  ushirikiano  yatakayojadiliwa kwenye mkutano huu yatahusu sekta za biashara na uwekezaji, usafirishaji, fedha, nishati, utalii, ulinzi na usalama uhamiaji, uvuvi na ardhi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 27 Januari, 2017

Post a Comment

Previous Post Next Post