Viuatilifu vinavyouma na kupuliza afya zetu

Dawa za kuua wadudu ama viuatilifu hutumiwa sana ulimwenguni kote ili kusaidia ukuaji wa mimea. Ingawa ni dawa zinazofaa, ila zina kemikali zenye sumu ambazo zinaweza kuharibu mifumo yetu ya ufahamu na mfumo wa neva.

Miaka 15 iliyopita, Tim Parton, meneja au bwana shamba wa shamba la Brewood Park huko Staffordshire nchini Uingereza, aliamua kuchukua hatua na kuanza kufanya majaribio ya kilimo cha kibaolojia.

Badala ya kutumia dawa za kuulia wadudu na mbolea, yeye huweka pembejeo za asili zinazojizalishaa zenyewe, kama vile trichoderma, na fangasi kwenye mimea yake, ili kuisaidia kukua na kurekebisha nitrojeni na fosforasi kwenye udongo.

Parton ni sehemu ya jumuiya ya wakulima inayokua inayofanya kilimo cha kupandikiza. Kilimo hiki ni mbinu mpya ya kilimo ambayo inatanguliza mbele udongo na afya ya mazingira kwa kupunguza pembejeo za syntetisk au zenye kemikali.

Alianza kutumia njia hii baada ya kuumwa na kichwa na kutokwa na vipele vya ngozi kutokana na kutumia viuatilifu vyenye kemikali.

Tangu aanze kutumia mbinu ya kilimo cha kibaolojia, Parton hajapata athari zozote za kiafya. Hajalazimika kutumia mbolea yoyote ya fosforasi na potasiamu kwenye mazao yake kwa zaidi ya miaka 10. "Ninajaribu kuweka mmea katika uwiano wa lishe niwezavyo, na ikiwa mmea umepata lishe sahihi, hauugui," anasema.

Ukubwa wa matumizi ya viuatilifu duniani

Dawa za kuua wadudu au viuatilifu ni vitu au kemikali zinazotumika kufukuza, kuharibu na kudhibiti wadudu, magugu au viumbe vingine vinavyoathiri ukuaji wa mimea.

Ingawa ni bora, dawa za kuulia wadudu zina kemikali zenye sumu ambazo zinaweza kuwa na athari kubwa, na wakati mwingine sugu kwa viungo vya hisia vya binadamu na mfumo wa neva.

Zilianza kutumiwa kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1930 ili kulinda mazao nchini Marekani, Jumuiya nyingi za kilimo hivi karibuni zinategemea matumizi ya dawa ama viuatilifu kwa sababu ya kusaidia sana kupata mavuno mengi. Leo, karibu theluthi moja ya bidhaa za kilimo duniani zinategemea dawa hizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna zaidi ya aina 1,000 za viuatilifu zinatumika duniani kote, huku baadhi ya aina zinazojulikana zaidi ni dawa za kuulia magugu (49%), za kuondoa ukungu na bakteria (27%) na viua wadudu (19%).

Mnamo 1990, matumizi ya viuatilifu duniani yalikuwa kilo bilioni 1.69; idadi hii ilikua zaidi ya asilimia 57% katika miongo miwili iliyopita, na kufikia kilo bilioni 2.66 mwaka 2020.

Ripoti ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa inatabiri kuendelea kukua kwa matumizi ya viuatilifu. Kwa kuwa idadi ya watu duniani inatarajiwa kufikia watu bilioni 9.3 ifikapo mwaka 2050, ongezeko la asilimia 60 la kiwango cha uzalishaji wa chakula linahitajika. Ili kuendeleza na kukidhi mahitaji haya, watafiti wanaamini wakulima watahitaji kutumia dawa ama viuatilifu vingi ziadi za kupambana na wadugu na magonjwa ya mimea.


Kulingana na utafiti wa mifumo ya kilimo ya Ulaya, kuacha kabisa dawa za kuua wadudu kunaweza kusababisha hasara ya asilimia 78% ya uzalishaji wa matunda, kupungua kwa mavuno ya mboga kwa 54% na hasara ya 32% ya mazao ya nafaka.

Lakini utegemezi wetu kwa dawa za kuulia wadudu pia huja kwa gharama kubwa kwa mazingira, na utafiti unaoonyesha dawa za kuulia wadudu zinaweza kuwajibika kwa upotezaji wa harufu katika nyuki wa asali, kuchafua vyanzo vya maji, na kutishia mifumo ya ikolojia ya majini.

Madhara kiafya

Viuatilifu ama dawa za kuulia wadudu zina madhara ukiila kupitia chakula au mazao yaliyotokana ama kukuzwa na kulindwa na dawa hizi. Madhara yake ni kupitia mchakato unaojulikana kama mlimbikizo wa kibayolojia. Hii hutokea wakati sumu inapoongezeka katika mwili kutokana na miili yetu kutokuwa na uwezo wa kuivunja. Kwa hivyo viuatilifu vingi vinaweza kurundikana katika mafuta mwilini.

Hii inaweza kuwa na athari mbaya kwa afya ya binadamu. Licha ya kanuni za kimataifa kuhusu matumizi ya viuatilifu, uchunguzi mmoja unakadiria kwamba visa milioni 385 hivi vya sumu kali ya viuatilifu bila kukusudia hutokea miongoni mwa wafanyakazi wa mashambani kila mwaka.

Inapopulizwa, dawa za kuulia wadudu huzalisha mvuke ambao unaweza kugeuka kuwa vichafuzi vya hewa. Nchini Marekani, asilimia 37-54% ya magonjwa yanayohusiana na dawa kati ya wafanyakazi wa kilimo yanahusishwa na kuvuta hewa ya dawa.

Dalili za mapema za kuathirika na dawa za kuua wadudu zinaweza kujumuisha maumivu ya kichwa, kichefuchefu, kizunguzungu na mfumo wa upumuaji, anasema Michelle Perro, daktari wa watoto wa zamani ambaye alianzisha shirika lisilo la kiserikali la GMO Science, jukwaa la umma ambalo madaktari hujadili na kuchambua athari za mazao na vyakula vilivyotengenezwa kwa vinasaba.

Athari za kiafya zinaweza kuwa kifafa hadi matatizo ya kupumua. Hali na matumiti ya muda mrefu wa aina ya dawa inayotumiwa pia husababisha athari kwenye mifumo yetu ya hisi na neva. "Kwa kuvuta viuatilifu kupitia mapafu inaweza kuwa sumu zaidi, kwa sababu utumbo wetu una vijidudu ambavyo husaidia kuondoa sumu," anasema Perro.

Dawa za viatilifu zinaweza kusababisha kupoteza harufi na uwezo wa machoment

Utafiti wa mwaka 2020 uligundua kuwa kati ya wafanyakazi wa kilimo wanaokadiriwa kuwa milioni 860 ulimwenguni, 44% wanaathiriwa na sumu ya dawa hizi kila mwaka. Hii ni kutokana na ukosefu wa vifaa vya kujikinga au kutumia vifaa vyenye kasoro, ambayo husababisha athari kupitia ngozi, kuvuta hewa au kumeza.

"Dawa za kuulia wadudu zinapoingia mwilini kwa kuvuta pumzi, [hupitia] kizuizi cha ubongo wetu wa damu na kudhoofisha utendakazi wa neva," anasema Chen. "Njia nyingine, [dawa za kuua wadudu] zinaweza kuingia katika mfumo wetu wa damu kupitia njia ya utumbo ikiwa zimemezwa ama kuliwa."

Tafiti nyingi pia huonyesha uhusiano kati ya matumizi ya dawa hizi na magonjwa ya mfumo wa neva. Dawa za kuulia wadudu zimehusishwa na hali kama vile ugonjwa wunaoitwa kitaalamu attention deficit hyperactivity disorder (ADHD) na ugonjwa wa Parkinson.

Parkinson ni ugonjwa wa ubongo ambapo mtu hukosa homoni ya dopamini. Hili hutokea baada ya seli zinazotengeneza dopamini kuharibika. Mtu mwenye ugonjwa huu anakuwa akitetemeka mikono (hand tremors), pamoja na shida ya kutembea. Huenda pia mtu akawa na shida za kufikiria.

Dawa za kuua wadudu wakati wa ujauzito au kwa watoto pia zinahusishwa na tatizo la usonji miongoni mwa watoto.

Kwa sababu zimeundwa kulenga tishu za neva za kiumbe, viua wadudu kama vile organofosfati, carbamates na viatilifu vya organochlorine ni sumu zaidi kuliko viua magugu.

Mnamo 2014, watoto wa shule moja waliathirika na sumu sumu hizi huko Bordeaux, Ufaransa. Katika shule hiyo ya msingi iliyo karibu na shamba la mizabibu, wanafunzi 23 walipata kichefuchefu, maumivu ya kichwa na kuwashwa kwa ngozi baada ya dawa za kuua kuvu kunyunyiziwa katika shamba hilo la mizabibu.

Hilo lilisababisha kutozwa faini ya dola $31,842 kwa mashamba mawili ya mizabibu yaliyohusika, baada ya kesi ya kibinafsi kuwasilishwa na vyama viwili vya mazingira vya Ufaransa Sepanso na Génération Futures.

Visa vya watoto kuugua kutokana na kuathiriwa na viuatilifu vinaweza kupatikana kote ulimwenguni, kutoka Hawaii hadi New Zealand. Nchini India, sumu ya dawa miongoni mwa watoto imekuwa suala muhimu la afya ya umma kwa miongo kadhaa sasa.

Chanzo; https://www.bbc.com/swahili/articles/cevyyk10ej1o.


Post a Comment

Previous Post Next Post