Je unaweza kupata saratani kwa kuzipaka kucha zako rangi ya jeli?


Wanawake maeneo mbalimbali Duniani wamekua wakiremba kucha zao kwa rangi mbalimbali za kuvutia.

katika upakaji wa rangi hizo, kuna aina mbalimbali ambazo hutumiwa.

Rangi ya jeli ni miongoni mwa aina ya urembo ambao wanawake hulazimika kukausha kwa kutumia kifaa maalumu ili iwezi kukauka na kukaa kwa muda mrefu katika kucha zao.

Rangi ya jeli ilianza kutumika kwa mara ya kwanza miaka ya 1980 lakini haikupata mafanikio wala umaarufu mkubwa kwa wakati huo.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni umaarufu wa rangi hii umekuwa mkubwa na matumizi yake yameshamiri kwa wanawake wengi Afrika Mashariki

Rangi hizi zina sifa za kung’aa zaidi inapopakwa katika kucha, kudumu kwa muda mrefu zaidi hata kama mpakaji atajihusisha na shughuli mbalimbali za kushika maji lakini pia hukauka hapo hapo mara baada ya kuingiza katika kifaa maalumu kwa ajili ya rangi hizo.

Kifaa hicho huchomekwa katika umeme na hutoa mwanga wa UV ambao husaidia kukausha kucha zenye rangi kwa muda mfupi tofauti na rangi ya kawaida ambayo haitumii mashine hiyo ili kukauka.

Na hapo ndipo wasi wasi unapoanzia kwani utafiti mpya unazua maswali juu ya mwanga unaotumika kukaushia rangi hiyo.

                                                 Kucha zilizopakwa rangi ya jeli

Utafiti unasemaje?

Hivi karibuni utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha California na Chuo Kikuu cha Pittsburgh ulielezea hatari inayoweza kupatikana kutokana na mwanga wa UV unaotoka katika kifaa cha kukaushia rangi ya jeli kuwa unaweza kusababisha saratani.

Utafiti huo ulitumia sampuli za seli za binadamu na panya kwa kuwamulikia mwanga huo wa UV kwa vipindi vya dakika 20 mara tatu mfululizo.

Dakika 20 za kwanza waligundua asilimia 20 hadi 30 ya seli zilikufa; baada ya kufanya vipindi vitatu vya dakika 20 karibu asilimia 65 hadi 70 zilikufa.

Utafiti huo umebaini kuwa hatua muhimu katika mchakato wa kukausha kucha zenye rangi ya jeli chini ya mwanga wa UV au LED inaweza kuharibu DNA na kusababisha mabadiliko katika seli za binadamu, inayohusishwa na hatari ya saratani.

Mwanga unaotoka kwenye mashine ya jeli unaweza kusababisha uharibifu wa DNA na mabadiliko katika seli za binadamu.

Je, utafiti huu unamaanisha nini hasa?

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam Dr Magreth Moshi anasema utafiti huu unatoa tu mwanga lakini hauwezi kukamilisha kuwa unaweza kuleta saratani.

“Kwasababu utafiti unatupa mwanga, na hatuwezi kupuuza utafiti na kwa kawaida mara nyingi unavyotumia mwanga ule ndivyo ambavyo unakuweka katika hatari ya kupata madhara”

Anasema kuwa utafiti unatoa njia ya kufanya tafiti nyingine zaidi ili kupata uhakika wa saratani hii ukijumuisha ushahidi wa muathirika ambaye amepata tatizo hilo kupitia vikaushia rangi hivyo.

Dkt.Magreth Moshi Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani

Uhusiano kati ya saratani na rangi ya jeli.

Hatua za kupaka rangi ya jeli ni sawa upakaji wa rangi ya kawaida, lakini baada ya kupaka jeli hutakiwa kuwekwa katika kifaa chake cha kukausha ambacho hutoa mwanga wa ultraviolet [UV] au LED ili kusaidia kuikausha na kudumu kwa muda mrefu.

Kila koti ya rangi ya jeli inahitajika kuwekwa katika kikaushio hiko kwa sekunde 30 hadi 60 kwa wakati mmoja.

Hatua hii ndio inayoweza kuleta madhara yatokanayo na mionzi ya UV.

Mwanga wa UV ni kama miale ya mwanga inayotoka kwenye jua, na kwa miaka mingi inajulikana kwamba mwanga wa UV unaweza kusababisha saratani ya Ngozi iwapo utaangaziwa na mwanga huo mara nyingi na kuchochewa na visababishi vingine kama umri.

Dkt. Magreth anasema kuwa mwanga wa mashine ya kukaushia jeli una nguvu zaidi hivyo husababisha kuharibika kwa DNA na kukuweka katika hatari ya kupata saratani.

Licha ya hilo pia hatari huongezeka kutokana na mara nyingi zaidi unavyotumia kukaushia rangi hicho

Kwahiyo Mara unazomulikwa na mwanga huo kwa njia yeyote hata kama sio kwa kifaa hicho cha kukaushia jeli kunaweza kuongeza hatari ya saratani katika ngozi iliyo wazi.

Je, Jamii hususani wanawake wanatakiwa kuwa na wasiwasi?

"Kutumia kifaa cha kukaushia jeli mara moja au mbili kwa mwezi inakuweka katika hatari ndogo ya kupata saratani," anasema Dr Magreth

Anasema utafiti huu haukuwa na majibu ya moja kwa moja kwani hauna takwimu za kutosha kuthibitisha hilo na haujafanywa katika sampuli ya watu wengi lakini umeonesha kwamba kunaweza kuwa na hatari hiyo.

“Waangalie mara wanaoenda kutumia vifaa hivi, ukifanya mara chache ni vizuri Zaidi kuliko mara nyingi, lakini pia tafiti zaidi zinahitajika kufanyika katika hili”

Ufanye nini kupunguza hatari inayoweza kutokea ya mwanga wa UV.


Wataalamu wa afya wanapendekeza baadhi ya tahadhari ili kupunguza hatari za kiafya ikiwemo kutumia mafuta maalumu ya kupunguza nguvu ya miale ya jua{Sunscreen} kupaka katika mikono kabla ya kuweka katika kifaa cha kukaushia rangi.

‘Lakini pia katika nchi zilizoendelea kuna glove maalumu kwa ajili ya kuzia huu mwanga wa hivi vikausha rangi wakati unatengeneza kucha zako kwa rangi ya jeli”

Anamalizia kwa kusisitiza kupunguza matumizi ya mara kwa mara ya vikaushia rangi hivi kwa maana ya kwamba unaweza kutumia mara chache.

Chanzo: BBC Swahil.com



Post a Comment

Previous Post Next Post