Kundi la Family Winners linaloongozwa na mwanadada aitwae Eunice Jery latoa msaada wa magodoro 32 kwa Watoto yatima.

Kikundi cha Winners Family  July 30, 2023 kimetembelea na kutoa msaada wa mahitaji maalumu wa chakula, vinywaji pamoja na magodoro katika kituo cha kulea watoto yatima cha Yoco kilichopo Mbezi Maramba mawili- Jijini Dar Es Salaam.

Akizungumza na blog ya jamii ya Habarika24, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Winners Family, Bi Eunice Jery, amesema kuwa wao kama wajasiriamali wanawake wameamua kurudisha fadhila kwa Jamii kwa kusaidia watoto yatima kupata mahitaji yao muhimu.
Amesema kuwa moja ya sababu iliyowafanya kurudi katika kituo hicho kwa mara ya pili ni kufuatia kukuta uhaba wa magodoro pamoja na vitanda ndani ya kituo hicho hapo awali hivyo kuwafanya wao kuweka ahadi ya kuja kutoa mahitaji hayo.

Pia amesema kuwa wametoa jumla ya magodoro 27 katika kituo hiko pamoja na vyakula kama mchele, tambi na vinywaji kama juice na maji ambapo vyote vimepokelewa na mwanzilishi wa Yoco Ndugu Joseph Ruzegama.

"Idadi ya magodoro tuliyoleta yanakidhi kwasababu kila mtoto atapata godoro moja, malengo yetu ni kusaidia watoto yatima, wagonjwa na wajane"
"Kila kitu ni wito kwenye maisha ya mtu, huu ni wito Mungu ameweka ndani yetu, mimi nilikuwa na ndoto ya kuwa na kikundi cha watu watakaokuwa wanafanya shughuli kama hizi za kurudisha kitu kwa jamii" alisema Eunice Jery.

Aidha pia kwa upande wa Mwanzilishi wa kituo cha Yoco, Ndugu Joseph Rugemaza, amesema kuwa wameufurahia ujio wa winners family kwa mara ya pili katika kituo chao kwasababu ni baraka na mioyo yao imeguswa.

Pia amesema kuwa wao kama kituo wanapokea mchango wa mtu binafsi na kutoka kwenye vikundi vya watu pia, huku wakiwa na watoto 32 hadi sasa ambapo mmoja amemaliza chuo kikuu mwaka huu kutoka katika kituo hiko.
"Tulianza na watoto watano lakini leo hii tuna watoto 32, haya ni mafanikio makubwa kwetu kwani kituo kinakuwa na tunafurahia kuona jamii inavyotusaidia katika malezi ya watoto kutimiza ndoto zao"
"Kufanya huduma ya kusaidia wahitaji inafanywa na watu maalumu ambao mioyo yao imeguswa kwasababu unaweza ukaishia njiani, inatakiwa moyo wako uguswe kusaidia wahitaji" Alisema Ndugu Rugemaza.

Kwa upande wa watoto wa kituo hicho wameelezea furaha yao ya kutembelewa na Winners Family kwa mara ya pili na kuendelea kuungwa mkono katika kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ili kutimiza ndoto zao za baadae.
Kikundi cha Winners family kimeanzishwa mwaka 2022, ambapo pia walipata nafasi ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa wanachama wao wawili pamoja na watoto wa kituo cha Yoco.



Post a Comment

Previous Post Next Post