MKURUGENZI TAMWA ZNZ:”TUANDIKE HABARI ZA KUPINGA UDHALILISHAJI ZITAKAZOLETA MABADILIKO KATIKA JAMII YETU”

Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Isaa akizungumza wakati wa uzinduzi wa utafidi wa kihabari ulifanywa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Shirika la UNESCO TanzaniaDkt.  Salum Suleiman Ali, mshauri elekezi wa utafiti wa masuala ya vitendo vya udhalilishaji uliofanywa na TAMWA ZNZ akiwasilisha ripoti.

Waandishi wa habari wametakiwa kuandika habari za udhalilishaji na ukatili wa kijinsi kwa kuzingatia vigezo vyote vya kiuandishi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

Hii itasaidia kujenga uelewa zaidi kwa jamii na kila taasisi inayohusika katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Akifungua mkutano wa kuwasilisha ripoti ya utafiti wa kihabari kuhusiana na uandishi wa habari za udhalilishaji kwa  vyombo vya habari, Mkurugenzi wa chama cha waandishi wa Habari wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) Dkt. Mzuri Issa amesema waandishi wa habari wanapaswa kuandika habari za udahililishaji kwa kina kwa kufuata taraibu zote za kiuandishi ili zilete mabadiliko katika jamii.

Aidha, Dkt Mzuri amewataka waandishi wa Habari kuisaidia jamii kubadilika na kuwa na uwezo wa kuwalinda watoto na wanawake ili kuona wanafikia ndoto zao.

Sambamba na hilo, Dkt Mzuri ameiomba serikali kuweka utaratibu wa kuwafanya wananchi waweze kumlinda mtoto na mwanamke dhidi ya vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kuweka sera na sheria ambazo zitaongeza nguvu ya kudhibiti vitendo hivyo.

 Amesema, “licha ya kuwepo sera na sheria lakini hazijawabana watu kuogopa makundi hayo na badala yake wanaendeleza matukio ya udhalilishaji.”

Amefahamisha kutokana na hali hiyo ipo haja ya kuwepo utaratibu maalum utakaowafanya wanaume kujiepusha na makosa ya udhalilishaji kwa kuepuka kuwadhalilisha watoto na wanawake.

Mapema akiwasilisha ripoti ya utafiti huo mshauri elekezi wa utafiti wa masuala ya vitendo vya udhalilishaji Dkt.  Salum Suleiman Ali amesema utafiti umeonesha taarifa hizo zinaripotiwa lakini bado kuna mapungufu ya ubora wa habari ikiwemo uchambuzi wa takwimu, uzingatiaji wa sera, sheria na mikataba ya kimataifa, mwendelezo wa habari na jinsi ya kuleta matokeo mazuri katika jamii.

Baadhi ya waandishi wa Habari waliofanya utafiti huo wa kihabari wamesisitiza kujifunza na kusoma zaidi pamoja na kufuata maadili na misingi ya kazi zao ili kufanya kazi  kwa ajili ya kuisaidia jamii.

Utafiti huo wa kihabari umefanywa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na shirika la UNESCO ukiwa na lengo la kuangalia jinsi waandishi wa habari wanavyoandika habari za udhalilishaji na namna ya kuonesha njia ya kukabiliana na changamoto  zinazojitokeza wakati wa kuzipoti.

Utafiti huo wa kihabari uliangalia habari za udhalilishaji zilizoandikwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia januari hadi machi, 2023 kwa vyombo vya habari ikiwemo, radio na magazeti.

 Utafiti uliangazia katika gazeti la Zanzibar Leo, Nipashe na Habari Leo, huku kwa upande wa redio uliangazia ZBC radio kupitia kipindi cha Habari za Mawio, Zenji fm, Assalam fm na Furaha fm.



 

Post a Comment

Previous Post Next Post