MBUNGE MAVUNDE KUWAPUNGUZIA MZIGO WA MALIPO YA MITIHANI YA MAJARIBIO WANAFUNZI DODOMA JIJI

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amenuia kufanya maboresho makubwa kwa kushirikiana na Jiji la Dodoma kwa lengo la kuinua elimu Jijini hapo ambapo moja ya maeneo ambayo ameyapa kipaumbele ni ununuzi wa mashine(photocopiers)kubwa 10 na kugawa kwenye Tarafa ili kuwezesha uchapishaji mitihani ya majaribio ya kila wiki na hivyo kupunguza gharama za uandaaji wa mitihani.

Mh Mavunde ameyasema hayo jana Jijini Dodoma wakati akizungumza na Wakuu wa Shule za Sekondari,Walimu wakuu wa Shule za Msingi na Maafisa Elimu Kata wa Jiji la Dodoma katika hafla ya kukabidhi mipira 400 iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na boksi 300 kutoka Shirika la Takwimu Nchini(NBS).
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya  sita chini ya Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa ambao umechochea ongezeko la udahili wa Wanafunzi.
Itakumbukwa kupitia mfuko wa Jimbo tuligawa mashine za kudurufu 5 kwenye tarafa na sasa nitaongeza tena mashine za kudurufu 10 kwenye tarafa zote ili kusaidia taratibu za uchapishaji wa mitihani ya majaribio.

Ni imani yetu kwamba kupitia juhudi hizi na za serikali taaluma ndani ya Dodoma Jiji itaendelea kukua na kuwafanya wanafunzi kufanya vizuri zaidi na kupata uelewa wa kutosha.Ili kupata nafasi ya kupanga mikakati vizuri,kuanzia mwaka huu nitaanzisha Teachers’ Breakfast Meeting ambapo viongozi tutakuwa tunakutana na walimu wote na wadau wa elimu mara mbili kwa mwaka kujipanga kuboresha elimu Jijini Dodoma”Alisema Mavunde

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Alhaji Jabir M. Shekimweri amewapongeza walimu na wadau wote wa elimu kwa mchango mkubwa wa kuiinua Dodoma Jiji kitaaluma na kuwataka kuongeza juhudi zaidi ili kufanya vizuri kitaifa.

Akitoa shukrani,Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Ndg. John Lipesi Kayombo ameishukuru TFF na NBS kwa michango yao ya mipira na chaki  ambayo itasaidia kukuza michezo na kuongeza ufanisi wa ufundishaji katika Jiji la Dodoma.

Post a Comment

Previous Post Next Post