KAMANDA JESHI LA ZIMAMOTO ASISITIZA UMUHIMU KUFATILIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA


Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani wakiwa katika majukumu ya kuokoa wahanga wa mafuriko Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani Mrakibu Mwandamizi Jenifa Shirima akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya kuwaokoa wahanga wa mafuriko Wilaya ya Rufiji

………….

NA NOEL RUKANUGA, PWANI

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani Mrakibu Mwandamizi Jenifa Shirima amewataka wakazi wa Mkoa huo kufatilia taarifa za hali ya hewa pamoja na kuchukua tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) jambo ambalo litasaidia kuokoa maisha yao kutokana mvua kubwa zinazonysha na kusababisha na mafuriko katika Wilaya ya Rufiji.

Akizungumza na mwandishi wetu leo April 15, 2024 Mkoani Pwani akiwa katika Opereshni ya uokoaji kwa wahanga wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji,  Mrakibu Mwandamizi Jenifa Shirima, amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka TMA mvua bado zinaendelea hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari.

“Taarifa kutoka TMA mvua zinaendelea, tafsiri yake maji yanaendelea kuongezeka, wakazi wa wilaya ya rufiji wanapofikiwa na boti za uokoaji wanapaswa kupanda boti hizo kwani serikali imeandaa utaratibu mzuri ili kuhakikisha watu wote wanakuwa salama pamoja na kupata huduma zote muhimu “ amesema Mrakibu Mwandamizi Shirima.

Mrakibu Mwandamizi Shirima amesisitiza umuhimu wa wakazi wa rufiji kutoa ushirikiano wa Askali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  wakati wakiendelea kutekeleza majukumu ya ukoaji ili kuhakikisha wanakuwa katika mazingira rafiki katika kipindi hiki cha mafuriko.

“Hapa kuna askali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakishirikiana jeshi la wananchi wakifanya uokoaji, hivyo watu wote ambao wamekwama katika maji wanapaswa kutoa taarifa ili waweze kupata msaada wa karibu, wanapofikiwa na boti za uokoaji wanapaswa kupanda“ amesema Mrakibu Mwandamizi Jenifa Shirima.

Amefafanua kuwa maeneo mengi yamezingira na maji…“Ukoaji unaendelea kwa njia mbalimbali ikiwemo maboti, nawatoa hofu wakazi wa wilaya ya Rufiji, waendelee kutoa ushirikiano kwa askali wanafanya uokoaji kwa kupanda katika maboti pamoja na kufatilia taarifa za hali ya hewa“ amesema Mrakibu Mwandamizi Shirima.

Hata hivyo Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA)  imeendelea kutoa  angalizo la uwepo wa mvua kubwa kwa maeneo machache ya Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani (Ikijumuisha visiwa vya Mafia) pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo April 15, 2024 kwa  vyombo vya habari imeeleza kuwa mvua hizo zitaendelea kunyesha hadi Aprili 19, mwaka huu, huku  wakitoa angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mavimbi makubwa yanayofikia mita mbili.


Post a Comment

Previous Post Next Post