Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari wa mitandaoni na bloga Desemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam.
...............................
KATIKA historia ya tasnia ya habari nchini Tanzania, yapo matamko ambayo hayapiti kama taarifa za kawaida, bali huacha alama ya kudumu. Kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuagiza waandishi wa habari za mitandaoni na blogs kulelezwa, kupewa fursa na kuwezeshwa ni miongoni mwa kauli hizo.
Hii si kauli ya kubembeleza, wala si ya kisiasa kwa ajili ya makofi; ni kauli ya kimkakati inayogusa mzizi wa mawasiliano ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kauli ya Msigwa Ndani ya Kikao Rasmi
Kauli hiyo ilinukuliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, Desemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati akifunga kikao cha pamoja cha wanachama wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA).
Kikao hicho kiliandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akizungumza ndani ya kikao hicho, Msigwa alieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahsusi kwa Wizara ya Habari pamoja na TCRA kuwalea vizuri waandishi wa habari za mitandaoni na blogs, kuwapa fursa na kuwawezesha ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi na ufanisi.
Mabadiliko ya Fikra ya Serikali
Kwa mara ya kwanza katika kiwango cha juu cha uongozi wa nchi, waandishi wa habari za mitandaoni wanatajwa si kama tatizo la kudhibitiwa, bali kama rasilimali ya kulelewa.
Ndani ya kauli hii kuna mabadiliko ya fikra: kutoka kwenye udhibiti kwenda kwenye ushirikiano, kutoka kwenye hofu kwenda kwenye imani, na kutoka kwenye mashaka kwenda kwenye uwekezaji wa muda mrefu.
Tasnia ya habari za mitandaoni imekua kwa kasi kubwa kuliko sera zake. Vijana wamejiajiri, wameunda majukwaa ya habari, wamejenga ushawishi, lakini mara nyingi wamefanya hivyo bila miundombinu ya kisheria iliyo rafiki, bila ulinzi wa kitaaluma, na bila mazingira ya kiuchumi yanayowawezesha kukua.
Katika mazingira hayo, kauli ya Rais Samia inakuja kama tunu, si kwa sababu tu imetamkwa, bali kwa sababu inaleta mwelekeo mpya wa namna serikali inavyotazama uandishi wa kidijitali.
Agizo lenye Tafsiri ya Kisera
Agizo kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na TCRA si dogo. Ni agizo linalobeba tafsiri nzito ya kisera. Kuwalea waandishi wa mitandaoni kunamaanisha zaidi ya kuwasajili au kuwatoza ada.
Kunamaanisha kuwaandalia mazingira ya kufanya kazi zao kwa weledi, kuwajengea uwezo wa kitaaluma, na kuwaona kama washirika wa maendeleo ya taifa, si kama wahalifu wa mtandaoni wanaosubiriwa makosa.
Ndani ya falsafa ya Serikali ya Awamu ya Sita, ushirikiano na wadau ndiyo nguzo kuu. Ndiyo maana kutajwa kwa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kama wadau wakubwa wa serikali si jambo la kawaida.
Huu ni uthibitisho kuwa serikali inatambua nguvu ya mitandao ya kijamii na blogs katika kusambaza taarifa, kujenga hoja za kitaifa, na kuwa daraja kati ya wananchi na mamlaka.
Changamoto Zinazohitaji Mageuzi
Hata hivyo, ni lazima kusemwa kwa uwazi kuwa kauli hii, pamoja na uzito wake, haitoshi peke yake. Waandishi wa habari za mitandaoni wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo gharama za usajili na leseni, ukosefu wa mifumo ya mafunzo endelevu, changamoto za kiuchumi, hofu ya adhabu kuliko mwongozo, pamoja na mazingira ya kisheria yasiyoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Ndiyo maana jukumu la Wizara ya Habari na TCRA halipaswi kuishia kwenye utekelezaji wa kawaida, bali liingie kwenye mageuzi ya mifumo. Kulea si kuadhibu, na kuongoza si kutisha. Utekelezaji wa maelekezo ya Rais unahitaji sera rafiki, taratibu zinazoeleweka, mifumo ya mafunzo, na majukwaa ya mazungumzo ya wazi kati ya serikali na waandishi wa habari za mitandaoni.
Wajibu wa Waandishi wa Mitandaoni
Kwa upande wa waandishi wenyewe, kauli hii ni fursa na pia ni mtihani. Ni fursa ya kuthibitisha kuwa wanastahili imani waliyopewa, na ni mtihani wa kuonesha uwajibikaji, maadili na weledi. Uhuru bila maadili ni hatari, na uwezeshaji bila nidhamu ni mzigo. Waandishi wa mitandaoni wanapaswa sasa kujiona kama sehemu ya taasisi pana ya habari, si wapita njia wa mitandao ya kijamii.
Rais Samia Suluhu Hassan pia amekuwa mstari wa mbele katika kutoa tuzo kwa waandishi wa habari kupitia Tuzo za Mama Samia. Hatua hii inapaswa kupongezwa, lakini ni lazima tuwe wakweli: tuzo pekee hazijengi tasnia imara. Zinapaswa kwenda sambamba na mifumo ya kuwawezesha waandishi kiuchumi, kitaaluma na kisheria.
Mwanzo Mpya au Kauli Tu?
Je, kauli hii imekuja wakati mwafaka? Ukweli ni kwamba imechelewa, lakini umuhimu wake haupungui. Tasnia ya habari za mitandaoni tayari ina ushawishi mkubwa, tayari inaathiri maamuzi ya kijamii na kisiasa, na tayari imekuwa chanzo cha riziki kwa maelfu ya vijana. Serikali haina budi kuikumbatia tasnia hii si kwa hofu, bali kwa hekima.
Mwisho wa yote, kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ni mwanzo wa ukurasa mpya kwa waandishi wa habari za mitandaoni na blogs nchini Tanzania.
Ni mwaliko wa kujenga tasnia huru, yenye uwajibikaji na mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya taifa. Lakini kama kauli hii itabaki kwenye hotuba bila mifumo madhubuti ya utekelezaji, historia haitakuwa na huruma.
Kwa sasa, kauli hii ni mwanzo mpya.
Ikiwekewa mifumo, itageuka kuwa urithi wa kudumu.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Bakari, akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, akizungumza.
Maafisa wa TCRA wakiwa kwenye kikao hicho
Mwendeshaji wa Blog ya Fullshangwe, John Bukuku akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Uchangiaji wa mambo kadha wa kadha ukiendelea.
Wanahabari wa mitandaoni wakiwa kwenye kikao hicho. Kutoka kushoto ni Frank Wandiba, Athuman Shomari na John Bukuku.
Blogers wakiwa kwenye kikao hicho. Kulia ni Mwendeshaji wa Blog ya Habari Faster, Emmy Mwaipopo.
Uchangiaji ukiendelea.
Mkurugenzi wa Magendela Blog, Hamisi Magendela (katikati) akiwa na Bloga wenzake kwenye kikao hicho.
Mwendeshaji wa Blog ya Kamanda wa Matukio, Richard Mwaikenda akichangia jambo kwenye kikao hicho.
kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea
ohn Marwa kutoka Jambo online Tv akishukuru baada ya kutoa mchango wake kwenye kikao hicho.
Imeandaliwa na Victor Bariety Simu;0757 856 284

Post a Comment