MSIGWA: WAANDISHI WA BLOG KABILIANENI NA WANAO WAITA DHAIFU


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa  akizungumza na waandishi wa habari wa mitandaoni na bloga Desemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam.

...............................

 

 Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

 

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka waandishi wa habari wa  mtandaoni kukabiliana na watu wanaowaita ni dhaifu katika kufanya kazi zao.

 

Msigwa aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa mitandaoni na bloga katika kikao kazi kilicho andaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kilichofanyika Desemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam.

 

“Waandishi wa habari nchini siyo dhaifu kama wanavyosema chukueni hatua ya kukabiliana nao kwa kuwajibu kulinda hadhi yenu msikae kimya,” alisema Msigwa.

 

Alisema waandishi wa habari wa mitandaoni siyo dhaifu na kuwa wanatekeleza wajibu wao ipasavyo na wana nafasi kubwa ya kutumia kalamu zao kujenga nchi.

 

Msigwa aliwahakikishia waandishi ulinzi wa serikali, akisema endapo sheria, kanuni au sera zitabainika kuwa kikwazo katika utendaji wao, zitafanyiwa marekebisho kwa maslahi mapana ya taifa.

Msigwa alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kulea na kuwawezesha waandishi wa habari wa mitandaoni na mabloga, badala ya kuwashughulikia kwa mtazamo wa adhabu, kujenga tasnia imara na yenye tija ya habari nchini.

 

Aidha, Msigwa, aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mwelekeo wake wa kulea wadau wa sekta ya habari badala ya kuchukua hatua kali za kinidhamu.

 

“ Mwelekeo huo unaendana na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo inalenga kushirikiana na wadau mbalimbali kwa manufaa ya taifa,” alisema.

 

Aliitaja Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kuwa ni wadau wakubwa wa serikali katika tasnia ya habari, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kusambaza taarifa na kujenga mawasiliano kati ya serikali na wananchi.

 

“Serikali imewaamini waandishi wa mitandaoni, sasa nanyi muendelee kuonesha imani kwa serikali. Ushirikiano wetu umeendelea kuimarika na changamoto zinazojitokeza tunazitatua kwa pamoja,” alisema Msigwa.

 

Alitangaza pia kuanza kwa maandalizi ya mafunzo kwa waandishi wa habari kwa kushirikiana na TCRA, akiwataka kuyapokea kwa mtazamo chanya kama sehemu ya kuongeza weledi na taaluma.

 

Kuhusu masuala ya kodi, Msigwa alisema serikali itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa mitandaoni, akitambua mchango wao katika kuitangaza nchi na kuvutia uwekezaji.

 

Aidha, alieleza kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ipo katika mchakato wa kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwawezesha waandishi wa habari, hususan wa mitandaoni.

 

Akizungumzia mazingira ya sasa ya kimataifa, Msigwa alisema vita vya dunia ya sasa vimehama kutoka silaha za kijeshi kwenda kwenye taarifa, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kulinda na kuipromote nchi.

 

Aliwahimiza waandishi kuhakikisha majukwaa yao yanatumika kulinda maslahi ya taifa na kuonya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao yanayoweza kuharibu taswira ya Tanzania.

 

Hata hivyo, Msigwa alionesha kusikitishwa na tabia ya baadhi ya waandishi kunyamaza wanapodhalilishwa, akiwataka kusimama na kulinda hadhi ya taaluma yao. 

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Bakari, akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, akizungumza.
Maafisa wa TCRA wakiwa kwenye kikao hicho
Mwendeshaji wa Blog ya Fullshangwe, John Bukuku akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Uchangiaji wa mambo kadha wa kadha ukiendelea.
Wanahabari wa mitandaoni wakiwa kwenye kikao hicho. Kutoka kushoto ni Frank Wandiba, Athuman Shomari na John Bukuku.
Blogers wakiwa kwenye kikao hicho. Kulia ni Mwendeshaji wa Blog ya Habari Faster, Emmy Mwaipopo.
Uchangiaji ukiendelea.
Mkurugenzi wa Magendela Blog, Hamisi Magendela (katikati) akiwa na Bloga wenzake kwenye kikao hicho.
Mwendeshaji wa Blog ya Kamanda wa Matukio, Richard Mwaikenda akichangia jambo kwenye kikao hicho.
kikao kikiendelea

Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea
ohn Marwa kutoka Jambo online Tv akishukuru baada ya kutoa mchango wake kwenye kikao hicho.
 

Post a Comment

Previous Post Next Post